Brighton & Hove Albion kuachana na Aisha Masaka

KLABU ya Brighton & Hove Albion inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini England haitaendelea na mshambuliaji wa Kitanzania, Aisha Masaka, msimu ujao baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Tangu ajiunge na timu hiyo msimu WA 2023/24 akitokea BK Hacken ya Sweden nyota huyo alicheza mechi mbili  kwa dakika 14 dhidi ya Arsenal (4) na Birmigham (10).

Sababu kubwa za Brighton kuchukua uamuzi huo zinatajwa kuwa ni kiwango ambacho mchezaji huyo amekionyesha pamoja na changamoto ya majeraha yaliyomsumbua kwa nyakati tofauti tangu ajiunge na klabu hiyo, hali iliyomfanya ashindwe  kuwa na mwendelezo.

Masaka alijiunga na Brighton akitarajiwa kuleta ushindani katika safu ya ushambuliaji, hata hivyo hali haikuwa rahisi kwake kutokana na majeraha pamoja na ushindani mkubwa wa nafasi ndani ya kikosi hicho.

Taarifa kutoka ndani ya menejimenti ya mchezaji huyo inaeleza Masaka tayari ana ofa kutoka klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi za Saudi Arabia na Hispania na wanaangalia uwezekano wa wapi atacheza.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa kipaumbele kikubwa kwa sasa ni kuchagua ofa yenye maslahi makubwa zaidi, sio kifedha pekee bali pia inayompa nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kurejesha kiwango chake.

“Brighton washamueleza kuwa watamuacha na hadi sasa hawajazungumza hivyo mchezaji mwenyewe aliamua amalize kwanza msimu kwa sababu huu ndio wa mwisho kisha atafute timu sehemu nyingine,” kilisema chanzo hiko na kuongeza

“Bado hakuna uhakika asilimia 100 kwamba ataenda wapi hadi sasa lakini wanaangalia mtonyo mzuri ila ofa ambazo ni nzuri na zimekubalika mezani ni kutoka Saudia na Hispania.”