Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema atawatumia wakaguzi wa wizara hiyo kukagua mahesabu ya vyama mbalimbali vya ushirika ili kubaini ubadhirifu.
Chongolo alisema hayo wakati wa mkutano mkuu wa 30 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), uliofanyika juzi na jana Jumamosi, Januari 10, 2026, jijini Dar es Salaam na kushirikisha wanaushirika zaidi ya 200 kutoka Tanzana Bara.
Alisema kwa sasa vyama hivyo vinatumia Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Coasco) kama mkaguzi wa nje, lakini pamoja na shirika hilo kufanya kazi nzuri, bado kunahitajika wakaguzi wengine ambao watatoa hati ya ukaguzi kutokana na mahesabu husika.
“Coasco inafanya vizuri sana katika kazi ya ukaguzi, hata hivyo bado kunahitajika wakaguzi wengine wa nje ili kuhakiki mahesabu na kutoa hati kama ni safi au la. Wizara yangu ina wakaguzi wengi ambao wanaweza kufanya kazi hiyo.”
“Nitakuwa natoa kibali cha muda cha kufanya kazi za nje ya ukaguzi kwa vyama vya ushirika ili kupata hali halisi ya mahesabu. Kazi ya hao wakaguzi haitakuwa mwisho, kwani na wao watakaguliwa na wakaguzi wengine ambao nitawapa kazi hiyo ili kupata hati ya mahesabu halisi,” alisema Chongolo.
Alisema vyama vya ushirika vinatakiwa kuendeshwa kwa weledi wa hali ya juu ili kupata maendeleo na kuchangia uchumi wa nchi.
Alisisitiza vyama vya ushirika vinatakiwa kuzingatia maadili na miiko ya uongozi ili kuimarisha utawala bora.
“Serikali ya awamu ya sita haitaki kuona vitendo vya ubadhirifu na ufujaji wa mali za ushirika vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wasio waadilifu,” alisema Chongolo.
Alisema Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wabadhirifu wote wa mali za ushirika kwa mujibu wa sheria za nchi.
Aliongeza viongozi wa ushirika wanapaswa kufuata misingi ya uaminifu na uadilifu ili kujenga taswira nzuri ya sekta ya ushirika na kuimarisha imani ya wanachama.
“Mimi binafsi nikiwa muumini wa ushirika niko tayari muda wowote kupokea na kushughulikia jambo lolote linalohusu ushirika, aidha sitakuwa tayari kuona mtu yoyote anakwamisha jitihada za kukwamua wananchi kupitia ushirika,” alisema.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Shirikisho na vyama vyote vya Ushirika kuhakikisha sekta hii inakuwa imara, endelevu na yenye mchango mkubwa katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Mbali na hayo, Waziri Chongolo alipongeza vyama vya ushirika kushiriki kikamilifu katika utaratibu unaowekwa wa kuwakinga wanachama na majanga mbalimbali kupitia Bima zilizopo na zitakazoanzishwa hasa bima za mazao.
Alisema kuwa bima hiyo itasaidia wakulima kuwa na uhakika wa shughuli zao za kilimo, kwani bima ni ulinzi halisi.
Pia Chongolo alivitaka vyama vya ushirika kushiriki kikamilifu kwenye utengenezaji wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Ushirika nchini (Cooperative Development Master Plan) kwa kuwa mpango huu ni kwa manufaa na sekta kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TFC, Tito Haule aliipongeza Serikali kwa kuchangia maendeleo makubwa ya sekta ya ushirika na sasa inakuwa moja ya nyenzo ya kuchangia maendeleo ya nchi.
Alisema TFC imedhamiria kuleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo. Alisema kuwa kwa kutambua mchango wa Taifa kupitia sekta ya ushirika, walianza kufanya kazi ya kuhakiki mahesabu na kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 10 wamefanikiwa kupata hati safi ya ukaguzi.
Haule alisema TFC imeweka mikakati mikubwa ikiwa pamoja na kuanzisha jukwaa maalum la kupata taarifa mbalimbali la Coop Talk, ambapo wana ushirika watalitumia kupata taarifa mbalimbali ikiwa pamoja na changamoto.
“Pia malengo yetu ni kuongeza wanachama na wigo wa TFC ili kuleta maendeleo zaidi kwa wanachama na kuchangia maendeleo ya Taifa,” alisema Haule.
Mtendaji Mkuu wa TFC, Fares Muganda alisema wataendelea kuendeleza sekta hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Alisema kuwa kazi yao kubwa kwa sasa ni kupanua wigo na kusisitiza kuwa wanachama kuendelea kujiunga katika bima ambayo kwa sasa zoezi hilo linafanyiwa majaribio katika wilaya tatu za mkoa wa Tabora.
Mrajis wa Vyama Vya Ushirika Tanzania, Dk Benson Ndiege aliitaka TFC kuwaunganisha wakulima na masoko ya kitaifa na kimataifa ya mazao yao sambamba na kurahisisha utekelezaji wa sera za Serikali katika kuwezesha usambazaji wa mbolea na pembejeo za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa sekta hiyo
Dk Benson alisisitiza umuhimu wa vyama vya ushirika kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima ili kuwasaidia kujikimu kimaisha kabla na baada ya mavuno lakini vilevile kudhibiti ulanguzi wa bei.
Pia aliwataka viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia kikamilifu usajili wa wanachama katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha ufikiwaji wa huduma za ushirika katika maeneo mbalimbali nchini.
