Arusha. Duka kubwa la kuuza vifaa vya umeme na elektroniki lililopo eneo Mtaa wa Bondeni jirani na Kituo Kikuu cha mabasi jijini hapa limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Jumapili na kusababisha hasara ambayo haijaelezwa mara moja.
Imeelezwa kuwa moto huo ulianza majira ya saa moja jioni ya siku ya Jumamosi, Januari 10, 2025 uliendelea kuwaka na kusababisha hofu ya kusambaa zaidi kutokana na eneo hilo kuwa na nyumba nyingi za biashara.
Duka hilo linamilikiwa na mfanyabiashara, Vitalis Timira anayejulikana kwa jina maarufu Mambo Leo, linauza vifaa mbalimbali zikiwamo Radio, televisheni, majokofu, kamera,simu na vifaa vingine huku uchunguzi wa chanzo cha moto ukiendelea.
Mrakibu Mwandamizi Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Jiji la Arusha, Oswald Mwanjegele akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi leo Jumapili, Januari 11, 2025 amesema thamani halisi ya mali zilizoteketea kwa moto hazijafahamika pia mmiliki na wafanyakazi wake walifanikiwa kuokoa sehemu ya mali.
“Tulipata changamoto ya kulifikia eneo lililoathirika kwa moto kwa sababu njia tulizotarajia zitatuwezesha kupenya zimegeuzwa stoo ya kuweka mizigo yao, hatua iliyofanya zoezi kukabiliana na changamoto wakati wa kukabiliana na moto huo,” amesema Mwanjegele.
Mwanjegele amewataka wafanyabiashara kuzingatia kanuni za usalama ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka Jeshi la Zimamoto.
“Jeshi la Zimamoto lipo wazi kwa wananchi na wafanyabiashara tushirikiane kuhakikisha hakutokei majanga ya moto na yanapotokea kuwe na mbinu za kudhibiti kabla moto haujaleta madhara makubwa ya uhai wa watu na mali zao,” amesema Mwanjegele.