Dunga wa CUF akomalia ushindi wa Ashatu Kijaji

Moshi. Haijaisha mpaka imaisha. Ni usemi unaoweza kuutumia kuelezea hatua ya mgombea ubunge Kondoa kwa tiketi ya Chama cha Civic United Front (CUF), Othman Dunga, kukimbilia kortini kupinga ushindi wa Ashatu Kijaji.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025, Kijaji (sasa Waziri wa Maliasili na Utalii) aligombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kutangazwa mshindi.

Hata hivyo, Dunga hakuridhishwa na matokeo hayo, akafungua shauri la uchaguzi namba 30257 la mwaka 2025 akipinga ushindi huo, akianisha sababu kuu sita, ikiwamo madai ya Kijaji kugawa baiskeli zenye nembo ya CCM na kutumia udini.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Januari 9, 2026 imetoa uamuzi kuhusu maombi ya dhamana ya gharama ya shauri hilo na kumwamuru Dunga kuweka dhamana ya Sh500,000 kwa kila mdaiwa.

Ni kutokana na uamuzi huo uliotolewa na Jaji Julliana Masabo, mdai atawajibika kuweka dhamana ya jumla ya Sh1.5 milioni kwa ajili ya wadaiwa watatu katika shauri hilo ambao ni Kijaji, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kondoa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika maombi namba 31994 ya 2025 ya kupunguziwa dhamana ya gharama za uchaguzi, Dunga aliomba apunguziwe kiwango kilichowekwa na sheria ambacho ni Sh5 milioni kwa kila mdaiwa ili aweze kulipa dhamana ya Sh750,000.

Alijenga hoja kuwa hawezi kumudu gharama za ukomo wa dhamana zilizowekwa na sheria kutokana na kipato chake kuwa kidogo, akieleza kabla ya uchaguzi alikuwa akihudumu kama Makamu Mwenyekiti CUF, nafasi ambayo haina mshahara.

Badala yake alikuwa akilipwa posho ambayo kabla ya uchaguzi mkuu ilikuwa ikitokana na chama kupokea ruzuku kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambayo kwa sasa haipo kwani chama hicho hakijapata sifa ya kisheria kupokea ruzuku.

Alieleza kutokana na uwezo wake mdogo wa kifedha, hata kampeni zake za uchaguzi ziliendeshwa kwa kutegemea michango kutoka kwa wananchi na wanachama wenzake, hivyo akaomba korti imuamuru alipe kiasi alichoomba.

Kijaji, msimamizi walivyopinga

Maombi ya Dunga yalipingwa na wajibu maombi wote kupitia viapo kinzani. Mjibu maombi wa kwanza (Kijaji) kiapo chake kilitolewa na Godwill Benda aliyetambulishwa kama wakili wake.

Kupitia kiapo hicho, alipinga hoja za mleta maombi akisema hakutaja wala kuthibitisha kiasi cha posho alichokuwa analipwa na wala hakuonyesha michango aliyokuwa akipokea wakati wa kampeni hizo.

Wajibu maombi wa pili (Msimamizi) na wa tatu (AG), hati yao ya kiapo kinzani ilitolewa na Wakili wa Serikali, Nixson Tenges, wakipinga maombi hayo wakitoa sababu zinazofanana na zilizotolewa na Kijaji.

Wakati wa usikilizwaji, Dunga aliwakilishwa na wakili wa kujitegemea, Masuna Kunju, huku mjibu maombi wa kwanza akiwakilishwa na wakili Cheapson Kidunge na AG akiwakilishwa na mawakili wa Serikali Erigh Rumisha na Nickson Tenges.

Akiwasilisha hoja za mleta maombi, Kunju alisisitiza hoja kuwa mteja wake hana uwezo wa kulipa kiwango cha ukomo wa dhamana ya gharama za shauri la uchaguzi ambacho ni Sh5 milioni kwa kila mdaiwa, sawa na Sh15 milioni.

Alieleza kiwango hicho ni kikubwa kulinganisha na kipato cha mleta maombi akirejea sababu alizotoa Dunga katika kiapo chake.

Akijibu hoja hizo, Kidumage alizipinga akieleza hazina mashiko kwani pamoja na kuwa mleta maombi anayo haki ya kusikilizwa kwenye shauri la msingi, haki hiyo inaambatana na wajibu ambao anapaswa kuutimiza kwanza.

Alisema wajibu huo ni pamoja na kuweka gharama iliyoanishwa na sheria.

Alieleza pamoja na kuwa mahakama ina uwezo wa kuamuru ulipwaji wa dhamana ya gharama pungufu, mwombaji lazima atimize vigezo kwa kuonyesha hana uwezo wa kuweka dhamana ya kisheria, jambo ambalo hajafanya.

Wakili alifafanua kuwa hoja kuwa mleta maombi alikuwa anategemea posho ilipaswa kuungwa mkono na ushahidi unaoonyesha kiasi gani cha posho alikuwa akilipwa, lakini kiapo chake kipo kimya, hakuonyesha michango aliyopokea.

Kwa upande wake, Rumisha hakuwa mbali na sababu zilizotolewa na Kidumage, bali aliongeza kuwa hakuonyesha ni kwa nini wanachama waliomchangia wakati wa kampeni, wasimchangie tena katika hatua hiyo.

Akitoa uamuzi kuhusu maombi hayo baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande zote mbili na kurejea sheria na uamuzi wa kesi mbalimbali, Jaji Masabo amesema anatambua maelezo ya kiapo ya mleta maombi ni ushahidi.

Hata hivyo, amesema katika mazingira ya shauri hilo, kukosekana kwa ufafanuzi na ushahidi wa kimaandishi unaounga mkono, kumeyaacha maelezo hayo kuwa hafifu, dhoofu na umeinyima mahakama kipimo halisi cha kutumia kupima.

Ni maelezo hayo ndiyo yangeipa mahakama kipimo cha kupimia kuamua iwapo kiwango cha Sh750,000 kilichoomba ni stahiki au la.

Jaji amesema kitendo cha kushindwa kuwasilisha taarifa ya michango ambayo mleta maombi alipokea kinaweza kutafsiriwa kuwa michango aliyopokea ni kidogo sana na sehemu kubwa ya kampeni hizo alizigharimia mwenyewe.

“Au kiwango alichopokea ni kikubwa sana na baada ya matumizi amebaki na bakaa ambayo ingemwezesha hata kulipa kiwango cha juu cha dhamana,” amesema.

Jaji amesema: “Isitoshe, kama walivyoeleza mawakili wa wajibu maombi, mleta maombi hajaieleza mahakama hii iwapo hana chanzo kingine cha mapato hali inayoleta hisia kuwa anacho au anavyo vyanzo vingine.”

“Kwa kuzingatia hayo yote, na ukweli kuwa dhamana haipaswi kuwa kizingiti cha kumzuia mleta maombi kupata haki yake ya kusikilizwa, ninaona dhamana ya gharama inayofaa kuwekwa kwe shauri hili ni Sh500,000 kwa kila mdaiwa,” amesema.

Dunga katika shauri la msingi la uchaguzi ambalo limepangwa kutajwa Januari 19, 2026 mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Silivia Lushashi, ameeleza sababu kuu sita zilizomsukuma kupinga ushindi wa Kijaji.

Anaiomba mahakama itoe tamko kuwa uchaguzi katika jimbo la Kondoa uliofanyika Oktoba 29, 2025 ni batili na ulitawaliwa na ukiukwaji wa sheria.

Pia, mahakama itoe tamko kuwa Kijaji hakuchaguliwa kihalali kuwa mbunge na anaiomba itoe amri ya kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Analalamika kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi, rushwa ilitolewa na mlalamikiwa wa kwanza na watu wake wa timu ya kampeni kwa ufahamu wake na ridhaa yake kwa nia ya kujipatia kura kutoka kwa wapigakura wa jimbo hilo.

Anadai wakati wa kampeni Oktoba 2025, Kijaji aliwaita baadhi ya wananchi kutoka Kata ya Pahi na kuendesha kikao katika Kijiji cha Pahi Madukani kisha akagawa baiskeli zenye nendo na rangi ya CCM kwa kila aliyehudhuria.

Mbali ya hayo, anadai Septemba 2025, Kijaji aliwakusanya wananchi kutoka vijiji mbalimbali vya jimbo hilo kwa nyakati tofauti na kuendesha kikao nao kisha kumpatia kila aliyehudhuria Sh20,000 na kuwataka wamchague.

Dunga anadai fedha na baiskeli zilizotolewa na mlalamikiwa kwa wapigakura zilileta ushawishi kwao kumchagua Kijaji na kutomchagua yeye na kusababisha anufaike na matendo hayo kwa njia ya kura ya Oktoba 29.

Anadai wakati wa kampeni maneno yaliyotolewa kwa niaba ya Kijaji, meneja wake wa kampeni na watu wanaounda timu ya kampeni, na kwa ridhaa yake, walitumia hoja za udini ili kujipatia kura kutoka kwa wapigakura.

Mlalamikaji anadai siku ya kupiga kura baadhi ya mawakala wake katika vituo vya kupigia kura walizuiwa kuingia kwa sababu ya barua ya utambulisho na viapo vyao na kulazimika kuacha kusimamia upigaji kura uliokuwa ukiendelea.

Anadai siku ya kupiga kura, baadhi ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi walipiga kura zaidi ya moja na kuzijaza katika masanduku ya kura zilizopigwa. Katika tukio moja, anadai mmoja wa wasimamizi wasaidizi alikamatwa.

Mlalamikaji anadai ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi na kasoro nyingine alizoziainisha ziliathiri uchaguzi wa ubunge jimbo la Kondoa na kuzuia uchaguzi wa mgombea ubunge ambaye ni chaguo la wapigakura wa Kondoa