MABOSI wa timu ya Express ya Uganda wamefungua mazungumzo ya kumrejesha aliyekuwa beki wa kushoto wa timu hiyo, Dissan Galiwango, baada ya nyota huyo kubakisha mkataba wa miezi sita na kikosi cha Dodoma Jiji unaofikia tamati Juni 30, 2026.
Galiwango aliyejiunga na Dodoma Jiji, Agosti 16, 2024, akitokea Kagera Sugar, alisaini mkataba wa miaka miwili na kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, ambapo hadi sasa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine, jambo linaloipa nguvu upya Express.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Dodoma Jiji, umeliambia Mwanaspoti Galiwango bado ana mkataba na kikosi hicho hadi mwishoni mwa msimu huu, ingawa suala la yeye kubakia au kuondoka litategemea na mapendekezo yote ya benchi la ufundi.
“Mkataba alionao unamruhusu kufanya mazungumzo na timu nyingine, lakini bado hatujafikia uamuzi wa mwisho, lengo letu kwa sasa ni kuhakikisha wachezaji wenye mikataba tunaendelea nao hadi mwishoni mwa msimu huu kwanza,” kilisema chanzo hicho.
Nyota huyo aliwahi kuichezea Express mwaka 2018, baada ya kuachana na Saints Mukono, huku akichezea pia timu mbalimbali za UPDF FC na Vipers zote za kwao Uganda, ambapo kwa sasa mabosi wa kikosi hicho wanapambana tena kumrudisha nyumbani.
Licha ya kucheza beki wa kushoto, Galiwango amekuwa na mchango mkubwa tangu atue katika Ligi Kuu Bara, akianzia kwa Kagera Sugar na sasa Dodoma Jiji, huku akionyesha kiwango kizuri kwenye uzuiaji na wakati huohuo pia timu ikishambulia.
