Kassim Mbarouk aanza vyema Uturuki

WINGA wa Kitanzania anayekipiga Dispas SC ya Ligi ya Walemavu Uturuki, Kassim Mbarouk ameanza vyema ligi hiyo baada ya kufunga bao moja na kuasisti moja kwenye mechi tatu alizocheza.

Mbarouk aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Parasports ya Tanzania, anakuwa mchezaji wa nne kutoka Tanzania kujiunga na Ligi ya Walemavu nchini Uturuki baada ya Ramadhan Chomelo, Shedrack Hebron (Sisli Yeditepe) na Mudrick Mohamed wa Mersin.

Akizungumza na Mwanaspoti winga huyo amesema licha ya kuanza vizuri, lakini anaamini bado hajaonyesha kiwango chake kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo mazingira.

Aliongeza kuwa ukiachana na mazingira hasa hali ya hewa, chakula ni kati ya vitu vinavyompa shida tangu amewasili kikosini hapo akifikisha takribani mwezi sasa.

“Ni kweli nimeanza vizuri kwa kupata nafasi ya kufunga bao na kuasisti, lakini bado sijaonyesha kiwango changu halisi kutokana na ugeni wa mazingira na vitu vingine,” amesema Mbarouk na kuongeza:

“Hali ya hewa ni tofauti na nyumbani, pia chakula kimenipa shida kidogo, lakini hayo ni mambo ya kawaida kwa mchezaji anayeenda kucheza nje ya nchi ninaendelea kujifunza na kuzoea taratibu ingawa sio rahisi.”