Mabadiliko bei ya mazao kudhibitiwa Kyela

Mbeya. Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Kyela mkoani Mbeya (Kyecu) kimesema mabadiliko ya mara kwa mara ya bei za mazao ya biashara, likiwamo zao la cocoa, yataanza kudhibitiwa baada ya kukamilika kwa viwanda vya uchakataji vinavyojengwa wilayani humo.

Kauli hiyo imetolewa kufuatia kushuka kwa bei ya cocoa hadi kufikia Sh12,250 kwa kilo moja katika mnada wa Januari 5 mwaka huu, ikilinganishwa na bei ya Sh26,000 kwa kilo moja iliyokuwapo takribani miaka miwili iliyopita.

Akizungumza leo Januari 11, 2026, Meneja wa Kyecu, Amani Hankungwe amesema licha ya kushuka kwa bei hiyo, chama hicho bado kipo juu ya bei elekezi ya Serikali ya Sh10,000 kwa kilo moja, hivyo kuendelea kulinda maslahi ya wakulima.

Hankungwe amesema mkakati mkubwa wa Kyecu ni kuhakikisha mchakato wa ujenzi wa viwanda vya kuchakata zao la cocoa unakamilika ndani ya miaka miwili ijayo, hatua itakayosaidia kuondoa mabadiliko ya bei yasiyotabirika na kuweka ushindani wa haki sokoni.

“Vipo viwanda viwili vinavyojengwa, kimoja cha mwekezaji binafsi na kingine cha chama chetu. Viwanda hivi vitachakata zao la cocoa, kuongeza thamani na kuwezesha upatikanaji wa bei shindani. Vitakapokamilika, tutakuwa na uhakika wa bei rasmi na wakulima watanufaika zaidi,” amesema.

Ameeleza kuwa kushuka kwa bei ya cocoa kwa sasa kunatokana na ushindani kutoka nchi za Afrika Magharibi, hususan Ivory Coast, ambazo zimeanza kuchakata zao hilo ndani ya nchi zao, hivyo kupunguza upatikanaji wa bidhaa ghafi kwenye soko la dunia na kuathiri bei ambayo Tanzania huuza.

Kutokana na hali hiyo, Hankungwe amewaomba wakulima na wananchi kwa jumla kuwa watulivu, akibainisha kuwa matarajio ya Kyecu ni kuona bei ya zao hilo ikipanda tena ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo, sambamba na kuongezeka kwa uwekezaji pindi viwanda vitakapokamilika.

“Tunataka kulinda thamani ya Kyecu baada ya kupata hati safi. Tumeongeza mazao matatu mengine katika mfumo wa stakabadhi ghalani ambayo ni ufuta, korosho na mbaazi,” ameongeza.

Aidha, amewahimiza wakulima kuongeza kasi ya uzalishaji na kuzingatia ubora wa mazao yao ili kuendelea kushindana kikamilifu sokoni na kunufaika na fursa zinazotokana na uwepo wa viwanda.

Kwa upande wake, mkulima wa zao la cocoa, Richard Haule, amesema mpango wa ujenzi wa viwanda hivyo utaondoa sintofahamu ya bei ambayo imekuwa ikibadilika mara kwa mara, akiuomba uongozi wa Kyecu kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

“Mkulima yeyote anataka kuona bei nzuri sokoni kwa sababu gharama za kilimo zimepanda kuanzia kukodi shamba, maandalizi hadi kuvuna. Kwa ujumla tunapongeza juhudi zinazofanywa na viongozi,” alisema Haule.

Naye mkulima mwingine, Judith Mwampamba amesema kukamilika kwa viwanda hivyo kutaleta ushindani miongoni mwa wanunuzi na hivyo kuongeza bei ya mazao na kumpa mkulima thamani anayostahili.

 “Isiwe zao la cocoa pekee, bali mazao yote yanayolimwa Kyela na yaliyopo kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani yapewe kipaumbele ili sisi wakulima tunufaike na kilimo chetu,” amesema.