Nguvu ya agano na Mungu mafanikio ya mwaka mpya

Dar es Salaam. Bwana Yesu asifiwe. Ninaitwa Mwalimu George Mbwambo, karibu katika mahubiri ya siku ya leo yenye kichwa kinachosema. ‘Nguvu ya agano kwa mafanikio ya mwaka mpya’. Tunapoanza mwaka mpya, kila mmoja wetu huwa na matumaini mapya, malengo mapya na ndoto za mafanikio.

Wapo wanaotamani mafanikio ya kiroho, kifamilia, kielimu, kiafya au kiuchumi. Hata hivyo, Biblia inatufundisha kuwa mafanikio ya kweli hayapatikani kwa nguvu zetu pekee, bali kwa kuingia na kudumisha agano la kweli na Mungu.

Agano ni ahadi ya kudumu kati ya Mungu na mwanadamu, inayojengwa juu ya utii, imani na uaminifu.

Maana ya agano katika Biblia
Agano ni makubaliano matakatifu. Katika Mwanzo 17:7, Mungu anamwambia Ibrahimu, “Nitalithibitisha agano langu kati yangu na wewe na uzao wako baada yako.” Hapa tunaona kuwa Mungu ni mwanzilishi wa agano, naye hulitekeleza kwa uaminifu.

Agano la Mungu halitegemei hali ya uchumi, siasa au mazingira ya jamii, bali hutegemea moyo wa mwanadamu kumpokea Mungu na kuishi kulingana na mapenzi yake.

Nguvu ya agano kwa mafanikio
Mafanikio yanayotokana na agano la Mungu yana msingi imara. Yoshua 1:8 inasema, “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako… ndipo utakapofanikiwa katika njia zako.”Mafanikio haya siyo fedha pekee, bali ni amani ya moyo, mwelekeo sahihi wa maisha na baraka zinazodumu. Watu wengi katika jamii yetu wanapambana na maisha kwa juhudi nyingi, lakini bila mwelekeo wa kiroho, juhudi hizo mara nyingi huzaa matunda ya muda mfupi.

Ukisoma Mwanzo 28:20-22 unaona Yakobo akiweka agano na Mungu la kumfanikisha katika safari yake na ukiendelea kufuatilia unamuona Mungu akimfanikisha kama walivyokubaliana. Hivyo ili ufanikiwe katika mwaka 2026 unahitaji makubaliano na Mungu yatakayomruhusu akufanikishe mwaka mzima katika safari yako.

 Ulinzi wa Kiungu: Mungu huwakinga walioko katika agano Naye. Zaburi 91:1-2 – Akaaye mahali pa siri pa Aliye Juu…

Mafanikio katika njia zako: Mungu huongoza hatua zako na kukupa ushindi. Kumb. 28:1-14 – Baraka za utii kwa wale wa agano.

Ushirika wa karibu na Mungu:Agano linafungua mlango wa uhusiano wa kipekee na Mungu. Yakobo 4:8 – Mkaribieni Mungu…

Nguvu ya kutimiza maono: Mungu hujitoa kutimiza kusudi lake ndani yako. Habakuki 2:3. Maono yatatimia kwa wakati wake.

Kibali mbele za watu: Kama kwa Yakobo na Yosefu, agano huleta kibali mahali pasipo tarajiwa. Mwanzo 39:21. Bwana alikuwa pamoja na Yosefu.

Baraka za kizazi: Agano linaathiri vizazi vyako kwa wema. Mwanzo 17:7. Agano la Mungu na Ibrahimu liliwahusu hata uzao wake.

Ufunguzi wa milango iliyofungwa: Mungu hufungua lango la mafanikio. Isaya 45:2-3. Nitakutangulia…

Moyo mpya na maisha ya utakatifu: Agano hubadilisha maisha ya mtu na kuleta utiifu. Ezekieli 36:26-27 – Nitawapa moyo mpya.

Agano na maisha halisi ya jamii
Katika jamii ya leo, tunaona changamoto nyingi: ukosefu wa ajira, migogoro ya kifamilia, rushwa, ulevi, na kukata tamaa miongoni mwa vijana.

Haya yote yanaonyesha pengo la maadili na mahusiano yetu na Mungu. Agano na Mungu linapotiliwa mkazo, hubadilisha mwenendo wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Mtu aliye katika agano na Mungu atachagua uaminifu kazini, upendo katika familia, na haki katika biashara. Hivyo, agano linakuwa suluhisho la changamoto za kijamii.

Wajibu wa mwanadamu katika agano
Mungu ni mwaminifu, mwanadamu ana wajibu wa kuitikia agano. Kumbukumbu la Torati 28 linaonyesha wazi baraka za utii na laana za kutotii.

Kwa mwaka mpya, tunapaswa kujiuliza: Je, tunaishi kulingana na neno la Mungu? Je, tunamheshimu Mungu katika maamuzi yetu ya kila siku? Maombi, kusoma Neno, na kutenda haki ni nguzo muhimu za kudumisha agano.

Agano kwa mwaka mpya
Mwaka mpya unahitaji ahadi mpya na Mungu. Siyo kwa maneno tu, bali kwa matendo. Kama familia, tunaweza kuanza kwa kusali pamoja. Kama vijana, tunaweza kuchagua maisha ya utakatifu.

Kama wafanyabiashara au wafanyakazi, tunaweza kuamua kufanya kazi kwa uaminifu. Zaburi 37:5 inasema, “Mkabidhi Bwana njia yako, umtumaini naye atatenda.”
Nguvu ya agano na Mungu ndiyo ufunguo wa mafanikio ya mwaka mpya.

Bila kumtanguliza Mungu, mipango yetu huwa dhaifu; lakini tukiwa katika agano naye, hata katika changamoto, tutasimama imara. Tuanze mwaka huu kwa kumweka Mungu mbele, tukijua kuwa agano lake ni chanzo cha baraka, mabadiliko na mafanikio ya kweli katika maisha yetu na jamii kwa ujumla. Amina.