Dar es Salaam. Ikiwa ni kutambua mchango mkubwa katika kuwapatia wahitimu wa vyuo vikuu fursa za mafunzo ya uzoefu wa kazi na ajira, Benki ya NBC imeibuka kinara kwa kutunukiwa Tuzo ya Mwajiri Bora katika Programu ya Mafunzo kwa Vitendo.
Tuzo hiyo imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira na kukabidhiwa jijini Dar es Salaam katika mkutano wa waajiri wanaotekeleza Programu ya Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi.
Hafla hiyo iliyofanyika jana Januari 10, 2026 ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali akiwamo Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Zuhura Yunus, maofisa kutoka OWM-KAM na wawakilishi wa taasisi mbalimbali.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo akizungumza na washiriki wa mkutano huo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mwakilishi wa NBC na Kaimu Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Grace Mgondah amesema heshima hiyo imetokana na utekelezaji thabiti wa programu ya mafunzo kwa vitendo, ambayo kwa kipindi cha miaka mitano imewezesha taasisi hiyo kuajiri takribani wahitimu 136 waliopitia mafunzo ya uzoefu wa kazi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Amesema kila mwaka takribani wahitimu 800,000 hadi 1,200,000 huingia kwenye soko la ajira nchini, huku changamoto kubwa ikiwa ni ukosefu wa ujuzi na uzoefu wa kazi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Zuhura Yunus akizungumza na washiriki wa mkutano huo.
Mgondah amesema programu hiyo imekuwa suluhisho muhimu kwa kuwajengea wahitimu ujuzi wa vitendo, uzoefu, maadili ya kazi na mtazamo chanya kuhusu ajira.
“Programu hii imekuwa chachu ya kuwapa wahitimu maandalizi halisi ya ulimwengu wa kazi, na kuwafanya waweze kushindana katika soko la ajira,” amesema Mgondah.
Ameongeza mbali na ajira za moja kwa moja ndani ya benki, imechangia kuwawezesha wahitimu wengine wengi kupata ajira katika taasisi mbalimbali, ambako wameendelea kufanya vizuri.
Kwa niaba ya benki hiyo, Mgondah ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupanua wigo wa programu hiyo ili kunufaisha wahitimu wengi zaidi.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu Benki ya NBC, Grace Mgondah (kushoto) aliwaongoza maofisa wa benki ya NBC kwenye tukio hilo.
Katika maelezo yake aliwahimiza wahitimu wote kujiandikisha kwenye mfumo wa OWM-KAM ili kuunganishwa na fursa mbalimbali za ajira kupitia jobs.kazi.go.tz.