Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametunuku nishani ya mapinduzi kwa watu maalumu na utumishi uliotukuka 18 katika kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, mipngoni mwao akiwemo Fatma Karume mke wa muasisi wa mapinduzi, Abeid Amani Karume.
Kati ya nishani hizo, wanane wamepewa za mapinduzi na nishani 10 za utumishi uliotukuka kwa viongozi na watumishi wa umma.
Hafla ya kutunuku nishani hizo imefanyika leo Jumapili, Januari 11, 2026 katika viwanja vya Ikulu, Unguja Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi, watumishi wa umma na ndugu za waliotunukiwa nishani hizo.
Akisoma tamko la kutunuku nishani hizo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Saleh Juma Mussa amesema hilo linafanyika kwa uwezo aliopewa Rais, chini ya kifungu cha 10 cha Sheria ya Mambo ya Rais Namba Tatu ya Mwaka 2020.
Amesema Rais anatunuku nishani za mapinduzi nane na nishani za utumishi uliotukuka 10 kwa viongozi, watumishi wa umma na watumishi wa sekta binafsi.
“Kati ya watunukiwa 18, wanne ni marehemu na wengine 14 wapo hai,” amesema.
Nishani ya Mapinduzi inatolewa kwa mtu ambaye aliasisi au alishiriki au aliyatukuza na aliyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Akitaja sifa za mtunukiwa, katibu mkuu amesema ni pamoja na kiongozi au mtu ambaye aliiletea sifa Zanzibar katika fani mbalimbali na kuonesha maadili mema ya kusifika na kuigwa.
Nishani iliyotukuka inatolewa kwa mtumishi wa umma au mtumishi wa sekta binafsi ambaye ametimiza utumishi wake kwa muda wa miaka isiyopungua 20 mfululizo au awe ametumikia utumishi usiofikia miaka 20 lakini katika utumishi wake huo amefanya jambo kubwa lenye kupigiwa mfano, masilahi kwa Taifa na katika kipindi chote hicho amekuwa na tabia njema.
Mtumishi huyo awe ametumikia Taifa kwa uzalendo wa hali ya juu na kufanya kazi kwa kujitolea , uwajibikaji uadilifu, ujasiri, na umakini katika kusimamia majukumu na utendaji kazi.
Waliotunukiwa nishani hizo ni Fatma Karume, hayati Sheikh Hassan Ameir Al Shirazy, hayati Sheikh Mussa Makungu Ali, Sheikh Saleh Omar Kaabi Ahmed, hayati Askofu John Ackland Ramadhan, Profesa Jose Piquer, Gulam Abdallah Rashid na hayati Mvita Mussa Kibendera.
Kwa waliopewa nishani ya utumishi uliotukuka ni pamoja na Brigedia Jenerali Saidi Hamisi Saidi (mkuu wa brigedi ya Zanzibar), CP Kombo Khamis Kombo (Kamishna wa Polisi Zanzibar) na Kanali Hassan Ali Hassan (Kamishna wa Uhamiaji)
Wengine ni Commodore Azana Hassan Msingiri (KMKM), Kanali Makame Abdalla Daima (Mkuu wa JKU), Kamishna Rashid Mzee Abdallah (Mkuu wa Zimamoto), Kamishna Khamis Bakar Khamis (Mkuu wa Magereza Zanzibar) na Kanali Burhan Zuberi Nassoro ( Kamishna Mkuu Mamlaka ya Kuzuia Dawa za kulevya), Luteni kanali Said Ali Shamuhuna (Mkuu kikosi cha valantia) na Ali Abdalla Ali (Kamishna Mkuu Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Dawa za Kulevya).