Dar es Salaam. Nani alimuua Farhan Maluli na mabaki ya mwili yaliyofukuliwa huko Sharifu Shamba jijini Dar es Salaam ni ya nani? Ndio swali linalohitaji majibu baada ya Mahakama ya Rufani kubatilisha hukumu ya kifo aliyopewa Hemed Ally.
Farhan ambaye alikuwa kondakta wa Basi la Kampuni ya Wahida Bus Services ilidaiwa aliuawa Juni 12, 2014 na Ally ambaye naye alikuwa kondakta wa Kampuni ya Mabasi ya No Rise Bus Services, akashitakiwa kwa mauaji hayo.
Kulingana na ushahidi wa mazingira uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri, kiini cha mauaji hayo kilitokana na mrufani Hemed Ally kupewa na marehemu Sh30 milioni ili amuagizie lori aina ya Fusso, lakini hakutimiza ahadi hiyo.
Ni kutokana na mvutano huo baina ya wawili hao, ndio mashahidi walidai mrufani aliamua kumuua Farhan akishirikiana na wenzake wawili ambao hawakupatikana, kisha wakauzika mwili wake na kwamba ni Ally ndiye alionesha walipomzika.
Mwili wake ulipatikana Februari 6,2015 ukiwa umezikwa ndani ya eneo la nyumba huko Ilala Sharifu Shamba Jijini Dar es Salaam zikiwa zimepita siku 239 tangu auawe lakini uchunguzi wa vinasaba (DNA), haukuthibitisha kama ni mwili wake.
Januari 9, 2025, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani iliyoketi jijini Dar es Salaam, Dk Mary Levira, Leila Mgonya na Gerson Mdemu lilibatilisha kutiwa hatiani na hukumu ya kifo aliyopewa Ally na kuamuru aachiliwe huru mara moja.
Ushahidi wa Jamhuri ulivyokuwa
Ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri ulidai kuwa Juni 12,2014, marehemu alielekea kituo cha mabasi kama ilivyokuwa siku zote lakini siku hiyo hakurejea nyumbani hivyo Juni 14,2014, mkewe Tatu Allu akatoa taarifa polisi.
Taarifa hiyo ilitolewa Kituo cha Polisi Kimara na uchunguzi ukaanza na katika uchunguzi huo ilibainika mrufani ndio mtu wa mwisho kuwa na mawasiliano na marehemu na mawasiliano yao yalihusu deni la Sh30 milioni alilokuwa anadaiwa.
Katika mahojiano ya awali, ilidaiwa mrufani alikiri kumuua marehemu akishirikiana na watu wengine wawili, ambao hawakupatikana, na wakauzika mwili wake katika nyumba iliyopo eneo la Ilala Sharifu Shamba jijini Dar es Salaam.
Ni kutokana nakukiri, ilidaiwa mrufani aliwaongoza polisi kwenye nyumba hiyo aliyoitaja ambapo eneo hilo lilifukuliwa mbele ya maofisa wa Polisi, viongozi wa Serikali ya Mtaa na matabibu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Katika ufukuaji huo, kulipatikana mabaki ya binadamu ikiwamo fuvu na mifupa mbalimbali pamoja na nguo zilizodaiwa ndizo alizokuwa amevaa marehemu siku anatoweka, pazia na chandarua ambavyo vilipelekwa MNH kufanyiwa DNA.
Mmiliki wa nyumba, Hamjan Nassoro aliyekuwa shahidi wa kwanza, alieleza namna mrufani alikodi nyumba yalipokutwa mabaki ya mwili na mkataba ulikuwa unamalizika Julai 15, lakini mrufani alisitisha mkataba miezi 5 kabla.
Alieleza kuwa Februari 2015, alipata wito wa Polisi kushuhudia ufukuaji katika nyumba ambayo alikuwa ameipangisha na kulipatikana mabaki ya binadamu.
Shahidi wa tatu, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Ronald Makona aliyekuwa mkuu wa upelelezi (OC CID), kituo cha Polisi cha Msimbazi, alidai Februari 6,2015, alifika shahidi wa tano, Sajini Alphonce na kudai mrufani anahusika na mauaji hayo.
Mrufani alikamatwa na kuandikishwa maelezo yake mbele ya wakili wake ambapo alikana kuhusika na mauaji lakini asubuhi ya Februari 9,2015, aliomba kikao naye na hapo aliangua kilio akisema yeye ndiye aliyemuua Farhan Juni 12,2014.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, mrufani alimweleza kuwa walimzika katika nyumba moja huko Sharifu Shamba, hivyo yeye na maofisa wengine wa polisi walikwenda na mrufani hadi eneo hilo ambako inadaiwa aliwaonyesha walipomzika.
Shahidi wa 9, Kaifunga Brais ambaye ni mkemia wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, alieleza alivyofanya uchunguzi wa DNA katika sampuli alizopelekewa lakini hazikuona hivyo haikuthibitika kama ni mabaki ya Farhan.
Mashahidi wengine ambao ni polisi walieleza namna walivyopeleleza tukio hilo na kushiriki katika ufukuaji huko Ilala Sharifu Shamba huku mashahidi ambao ni raia walieleza uhusiano baina ya marehemu na mrufani na madai ya Sh30 milioni.
Katika utetezi wake, mrufani huyo alikanusha mashitaka hayo lakini akakiri kumfahamu Farhan na kwamba wakati tukio hilo linatokea alikuwa safarini Zanzibar na kwamba aliteswa na polisi ili kusaini maelezo ya onyo ya kukiri kosa.
Ni kutokana na ushahidi huo,Oktoba 17,2022, Hakimu mkuu mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwenye mamlaka ya nyongeza, Joyce Minde, alimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo, ambayo aliikatia rufaa kuipinga.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa, wakili Jeremia Mtobesya na Sweetbert Nkuba walimwakilisha mrufani na walijenga hoja za kisheria kuwa upande wa Jamhuri haukuwa umethibitisha shitaka bila kuacha mashaka kama sheria inavyotaka.
Katika wasilisho lake, wakili Mtobesya alisema hakimu Minde alipuuzia uwezekano kwamba inawezekana ni mtu mwingine ambaye alitenda kosa hilo au kwamba mabaki yale ya mwanadamu yaliyofukuliwa hayakuwa ya Farahani.
Alisisitiza kutiwa hatiani kwa mrufani kuliegemea ushahidi wa mazingira, maelezo ya onyo ya mrufani ya kukiri kutenda kosa na maungamo yake ya mdomo.
Alisema ingawa maelezo hayo yalipokewa kama kielelezo, lakini upokewaje wake haukukidhi vigezo vya kisheria, mrufani hakuonywa kikamilifu na akatilia shaka kama wakati anatoa maelezo hayo alikuwa ni mtu huru.
Wakili Mtobesya alisema maelezo ya mdomo ya kukiri kosa yalihitaji kuungwa mkono (corroborative) na ushahidi mwingine ili kuufanya uaminike lakini hapakuwepo na ushahidi wowote unaounga mkono ushahidi huo wa mdomo.
Lakini alisema kulikuwa hakuna msingi wa ushahidi kuthibitisha kuwa mwili ule uliofukuliwa Ilala Sharifu Shamba ulikuwa ni wa Farhan kwa kuwa uchunguzi wa DNA haukuoana na sampuli za DNA zilizochukuliwa kutoka kwa watoto wake.
Jamhuri kwa upande wao, kupitia kwa wakili mwandamizi wa Serikali, Ashura Mnzava, akisaidiana na wakili wa Serikali, Agnes Mtunguja walipinga rufaa hiyo lakini akakiri kuwa kesi hiyo imejengwa katika ushahidi wa mazingira.
Alieleza kuwa yapo mazingira yanayomlenga mrufani na tukio hilo ikiwamo kusitisha ghafla mkataba wa nyumba, uwepo wa mgogoro wa fedha na hata alipoitwa Polisi, alisita kwenda akihofia kukamatwa kwa kosa hilo.
Wakili Mnzava alikiri kuwa, DNA haikuthibitisha ni mwili wa Farhan lakini ushahidi wa mazingira unaonesha ni mabaki ya mwili wake kwani ni mrufani ndiye aliyewaongoza polisi eneo alipozika na pia vitu vilivyopatikana eneo hilo.
Katika hukumu yao, majaji waliosikiliza rufaa hiyo kwa sehemu kubwa walikubaliana na hoja za wakili Mtobesya ambaye alijenga hoja kuwa wakati mrufani anatoa maelezo yake ya onyo na kukiri kosa hakuwa mtu huru.
Majaji hao walisema kumbukumbu za kesi hiyo zinaonesha wazi kuwa, maelezo yake ya kwanza aliyoyaandika mbele ya wakili wake alikana kutenda kosa hilo lakini siku iliyofuata akaandika maelezo bila kuwepo wakili na kukiri kosa.
“Kuna jambo haliko wazi kwamba kwanini mrufani kama kweli alikuwa tayari kukiri kosa kwanini hakupelekwa kwa mlinzi wa amani akaandike maelezo ya ungamo”
“Zaidi, tumebaini kuwa maelezo yake ya awali ambayo hayakutolewa kama kielelezo aliyaandika mbele ya wakili wake na akakana kuhusika. Lakini maelezo hayo yalipaswa kuungwa mkono na ushahidi mwingine,”walieleza Majaji.
Majaji hao walisema hoja ya wakili Mtobesya ni kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa mabaki yale ni ya mwili wa Farhan, lakini wakili Mnzava ametoa mtiririko wa matukio ya mrufani ambayo yanathibitisha ndiye mhusika.
Moja ni kusafiri kwenda Zanzibar mara tu baada ya Farhan kutoweka, mbili ni mrufani kushidwa kuripoti polisi alipopewa wito, kufanana kwa mapazia yaliyopatikana kwa mama yake yakifanana na yaliyopatikana eneo la tukio.
“Kwa masikitiko, tunaona kwamba madai haya ni ya kutiliwa shaka tu na hayana uthibitisho unaohitajika kuunda ushahidi wa kimazingira,”walisema majaji hao.
Majaji walisema hakimu aliyemtia hatiani aliegemea maelezo ya onyo kumtia hatiani mshitakiwa lakini baada ya kupitia kumbukumbu za kesi wamebaini yalipokewa kama utambulisho tu (identification purposes) na sio kielelezo.
Kwa mujibu wa majaji hao, kielelezo ambacho hakikupokewa na Mahakama kama kielelezo cha kesi hakiwezi kujenga msingi wa hukumu hivyo wanaona hakimu alikosea kisheria kutumia maelezo hayo kumtia hatiani mrufani.
Ni kutokana na hoja hizo, majaji hao walibatilisha kutiwa kwake hatiani na kufuta adhabu ya kifo aliyopewa na wakaamuru mrufani achiliwe huru mara moja isipokuwa tu kama anashikiliwa mahabusu kutokana na sababu nyingine.
