UHAKIKA ni kwamba Yanga itakuwa na kiungo mpya, Allan Okello, msimu huu baada ya dili lake kukamilika zikitumika saa tatu kupambana kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa sawa. Okello anaichezea Vipers ya Uganda.
Rais wa Yanga, Hersi Said ambaye ametumia siku moja wiki hii kwenda Uganda kumaliza dili hilo kisha akarudi fasta Unguja, Zanzibar, kushuhudia timu hiyo ikitinga fainali za Kombe Mapinduz kwa kuichapa Singida Black Stars kwa bao 1-0.
Juzi, Yanga ilikata tiketi ya kucheza fainali za Mapinduzi na jukwaani Hersi alikuwepo akiwasili dakika chache akitokea Uganda kumaliza dili hilo ambalo lilikuwa gumu kukamilika.
Hersi alilazimika kusafiri hadi Uganda kulazimisha dili hilo baada ya kocha Pedro Goncalves kuonyesha uhitaji wa kiungo huyo.
Taarifa kutoka Uganda zinaeleza kwamba, Hersi hakuwa na kikao rahisi na rais wa Vipers, Lawrence Mulindwa ambaye awali aliweka ngumu kumuachia kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa uwanjani akiwa pia anaitumikia timu ya taifa ya Uganda.
Mulindwa aligomea ofa mbili za Yanga ile ya kwanza Dola 50,000 na ya pili 100,000, lakini akalazimika kuchukua Dola 120,000.
Licha ya utata wa Mulindwa, lakini alikubali dakika za mwisho kumuachia Okello ambaye amebakiza miezi sita kwenye mkataba na Vipers.
Taarifa kutoka Vipers ni kwamba Mulindwa alikubali ushawishi wa Hersi kwa kuheshimu hatua ya bosi huyo kusafiri mpaka Uganda kwa ajili ya suala hilo.
Urahisi wa Hersi ulitokana na uamuzi wa Okello mwenyewe kumwambia Mulindwa kwa simu kwamba anahitaji changamoto mpya na kwamba, amalizane na rais huyo wa Yanga.
Okello wakati wowote kuanzia sasa atasaini mkataba wa miaka miwili na nusu kuwa mchezaji mpya wa Yanga baada ya makubaliano ya pande mbili kwa klabu kukamilika.
Hata hivyo, hataweza kucheza mechi nne za makundi za Yanga kwani tayari alishacheza mechi hizo akiwa na Vipers iliyoishia hatua ya awali.
