SERIKALI YAKABIDHI VITABU 5,000 VYA ELIMU YA DINI YA KIISLAMU

:::::::::::

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amekabidhi vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa ngazi ya sekondari kwa Taasisi ya Kusimamia Ufundishaji wa Elimu ya Dini ya Kiislamu (TISTA), ikiwa ni hatua ya kuimarisha ufundishaji wa somo hilo nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika jana katika ofisi za Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) jijini Dar es Salaam, ambapo Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, akiongozana na viongozi wengine wa dini, alipokea vitabu hivyo kwa niaba ya TISTA.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mkenda alisema Serikali imekabidhi jumla ya nakala 5,000 za vitabu vya kiada vya Somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa shule za sekondari, vyenye thamani ya Sh milioni 16, pamoja na nakala 1,000 za vitabu vya mwongozo wa mwalimu vyenye thamani ya Sh milioni 1.2. Alisema jumla ya vitabu vilivyokabidhiwa vina thamani ya Sh milioni 17.2.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akizungumza kabla ya kukabidhi vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa ngazi ya sekondari.

Prof. Mkenda alisema Serikali itaendelea na zoezi la uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa ngazi ya kidato cha sita, pamoja na vile vilivyobaki vya kidato cha tatu na cha nne mara vitakapokamilika. Aliongeza kuwa, BAKWATA itapatiwa nakala kadhaa kwa ajili ya kusambaza katika shule zisizo za umiliki wa Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo aliishukuru Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na TISTA, hususan katika kugharamia kazi za uandishi na uidhinishaji wa vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini nchini ili kuhakikisha Elimu ya Dini inafundishwa kwa viwango vinavyostahili na kuchangia katika kumjenga Mtanzania mwenye maadili mema.

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi akizungumza Leo wakati wa makabidhiano ya  vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa ngazi ya sekondari kwa Taasisi ya Kusimamia Ufundishaji wa Elimu ya Dini ya Kiislamu (TISTA).

Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, aliishukuru Serikali kwa ushirikiano wake mkubwa uliowezesha kukamilika kwa zoezi la uandaaji wa maudhui ya vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu, akisema hatua hiyo itaongeza ubora wa ufundishaji wa somo hilo shuleni.