Tchakei achomolewa Yanga, sababu yatajwa

LICHA ya kutajwa kumalizana na Yanga, kiungo mshambuliaji raia wa Togo, Marouf Tchakei, anarejea Singida Black Stars baada ya mpango wa kujiunga timu hiyo ya Jangwani kwa mkopo kugonga mwamba katika dakika za mwisho.

Tchakei ambaye alikuwa amejiunga na Yanga na kutumika katika mechi moja ya mashindano Zanzibar hatakuwa sehemu ya kikosi hicho ikielezwa kuna mambo hayajaenda vizuri.

Wakati ikielezwa hivyo, Mwanaspoti limezinasa za ndani kuwa uwezekano wa kiungo huyo kuitumikia Yanga ni mdogo kutokana na sajili mbili zilizofanyika hivi karibuni ndani ya timu hiyo kuongeza idadi ya nyota wa kigeni.

Yanga imekamilisha usajili wa straika Leonardo Depu na kiungo mshambuliaji Allan Okello ambaye awali ilimkatia tamaa baada ya kuwaniwa na timu mbalimbali, lakini rais wa kikosi hicho cha Jangwani, Hersi Said amemaliza dili hilo, hivyo atavaa uzi wa njano na kijani.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa baada ya kukamilika kwa dili hilo mpango wa kuwa na Tchakei umekufa na kuamua kumrudisha Singida Black Stars.

“Ni kweli Tchakei hatakuwa sehemu ya kikosi kutokana na kukamilika kwa dili la Okello ambaye tuliamini kuwa hatutaweza kumpata kutokana na ugumu tuliokutana nao, lakini mambo yameenda vizuri, hivyo hatuna sababu ya kujaza wachezaji wengi kikosini,” kilisema chanzo.

“Hata hivyo Tchakei hatukuwa tumemsajili, kocha aliomba kumuangalia kupitia mashindano ya Mapinduzi na ndio maana hatukumtangaza kama ilivyokuwa kwa Mohammed Damaro.”

Mwanaspoti linajua kwamba Yanga imeamua kuachana na Tchakei kwani tayari nafasi za wachezaji wa kigeni zimejaa.

Kukwama kwa dili hilo kunamaanisha kuwa Tchakei ataendelea kuitumikia Singida Black Stars katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara badala ya kuvaa jezi za mabingwa hao watetezi.