Trident yagoma kumuachia Sichone | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI kinda wa Kitanzania, Mourice Sichone yupo kwenye mvutano baada ya klabu anayoitumikia Trident FC ya Zambia kukataa kumuachia, huku mchezaji huyo akionyesha nia ya kurejea nyumbani Tanzania.

Kinda huyo (18) alisajiliwa katika dirisha dogo msimu uliopita akitokea Mpulungu Harbour FC ya nchini humo alikocheza mechi 12 na kuhusika katika mabao tisa akifunga manne na kuasisti matano.

Sichone ambaye bado ana mkataba na Trident uliosalia wa miezi mitatu, kwa sasa anafanya mazoezi na Namungo, klabu ambayo imempa ofa ya mkataba wa miaka miwili.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Namungo, klabu hiyo inaamini katika uwezo wa mshambuliaji huyo na inaona anaweza kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji, hasa kutokana na umri wake mdogo na kasi aliyonayo.

Hata hivyo, juhudi za Namungo kumpata mchezaji huyo zinakabiliwa na changamoto hiyo baada ya Trident kusisitiza kuwa bado inamhitaji na haiko tayari kumuachia kwa sasa hadi atakapomaliza mkataba wake.

SICHO 01

“Kocha amevutiwa na uchezaji wake na hata wachezaji wamemkubali, lakini shida ni barua ya kumuachia kule ndio changamoto. Namungo wanapambana kuhakikisha kabla ya dirisha kufungwa Januari 31 awe tayari amesajiliwa,” amesema mmoja wa viongozi.

Chanzo cha karibu na mchezaji huyo kimeeleza kuwa Sichone mwenyewe ana nia ya kurudi Tanzania, akiamini kuwa atapata nafasi kubwa zaidi ya kucheza mara kwa mara.

SICHO 02

“Sichone anataka kucheza zaidi na kuwa karibu na familia. Anahisi Ligi Kuu itampa fursa hiyo kwa sasa, lakini kuna changamoto za nje ya uwanja alizopitia hataki kurudi tena Zambia,” kilisema chanzo hicho.

Kwa sasa, hatma ya mshambuliaji huyo bado haijafahamika wazi, huku mazungumzo yakiendelea kati ya pande zote mbili ili kupata suluhu itakayomridhisha mchezaji pamoja na klabu zote mbili.