Canada. Kwa wenyeji wa mwambao hasa mijini wanajua tutakachoongelea leo. Hii hutokea baada ya kuwa na migogoro katika ndoa.
Waathirika wengi wa uchafu na utapeli huu ni kina mama. Hivyo, tunawaasa kuwa wachunge na wasome hii makala kwa umakini.
Kuna kitu cha kipumbavu, kipuuzi na kitapeli kinachoitwa kuchezewa via vya uzazi. Tunadhani tunaeleweka. Mchezo huu hatari na mchafu huchezwa na waganga wa kienyeji. Wapo waganga wanaodhalilisha kwa kujifanya mabingwa wa kuongea na majini, kusomea watu dua za kuwasafisha na mambo mengine kama haya.
Kuna kisa kama hiki kilitokea jirani yetu wakati tukiishi Dar es Salaam. Mama mmoja mjinga aliyekuwa akitapatapa kuokoa ndoa yake alikwenda kwa mganga wa kienyeji kutaka msaada asijue hakuna dawa ya mapenzi.
Baada ya kuhojiwa na mganga huyu tapeli na mharibifu aliyejua siri za mhusika, alimwambia kuwa alikuwa amechezewa via vya uzazi. Mama alishangaa. Aliuliza nini dawa ya kutibu tatizo hili.
Bila aibu, yule tapeli alimwambia kuwa alikuwa amechezewa via vya uzazi na shangazi yake kutokana na wivu wa mafanikio yake kielimu. Hivyo, alimmwambia kuwa aende atafute mwamaume ambaye si mumewe ampe dawa ajipake na kushiriki naye ngono.
Pamoja na kushangaa, tatizo la huyu mama mjinga na mwenye kutapatapa liliongezeka. Swali lilikuwa, je, angempata wapi mtu wa kufanya kitendo hiki cha ovyo?
Bila kufikiri madhara ya tendo hili, yule mama alimwambia yule mganga mwanaume kuwa hakuwa na mtu wa kuweza kufanya kitendo hiki.
Mtego wa tapeli huyu mharibifu ulikuwa umenasa. Kwani, alimwambia kuwa yeye angefanya kazi hiyo kama angeongeza malipo ya huduma yake kwake. Mama, kwa ujinga na kutapatapa, licha ya kuamini upuuzi huu, aliridhia. Siku ilipofika, alijiandaa na kwenda kwa tapeli huyu ambaye alikuwa na chumba cha kufanyia shughuli zake kando ya nyumba yake. Wawili walijifungia ndani na kufanya uchafu wao huku mama akiamini alikuwa amepata tiba kumbe ndo alikuwa amekuza tatizo.
Wakiwa wamemaliza mambo yao, yule tapeli aliongeza masharti. Alisema kuwa kwa vile majini yatakuwa yamechukia, alipaswa aongeze dau. Matatizo yalizidi kuongezeka.
Yule tapeli aliongeza masharti kuwa, kwa kuangalia vifaa vyake, ilibidi wafanye ngono kwa mwezi mzima hadi atakapojiridhisha kuwa mteja wake angekuwa amepona. Yule mama alistuka na kuuliza mbona aliambiwa wangefanya mara moja tena kwa kuingia kidogo tu na si kufanya japo jamaa alifanya alivyotaka hadi akamaliza? Jamaa aling’aka kuwa hayo yalikuwa si maagizo yake bali majini.
Yule tapeli alishikilia msimamo wake. Aliongeza sharti kuwa kama angekataa, angemtafuta mume wa mhusika aombe radhi kwa kufanya naye mapenzi.
Badala ya kutibiwa, yule mama mpumbavu alijikuta kaingia mtego na kwenye tatizo kubwa zaidi ya lile lililokuwa limempeleka na kumuingiza kwenye uchafu huu. Kitu ambacho huyu mama hakujiuliza ni inakuwaje uchafu unaondolewa na uchafu zaidi.
Kufupisha kisa hiki kirefu, baada ya tapeli ambaye, kwa bahati mbaya, alikuwa akijuana na mumewe alishikilia kuwa angekwenda kuomba msamaha. Baada ya maji kuzidi unga, yule mama aliamua ajishitaki kwa mumewe.
Kabla ya kufanya hivyo, alimuuliza mumewe “hivi nikikwambia kosa nililofanyiwa utanisamehe?” Mume kwa kutojua, alisema “hakuna tatizo we sema tu.”
Si ndipo mama akajilipua kwa kudai kuwa alikwenda kwa mganga kuulizia dawa ya tumbo akambaka. Mume hakuamini. Alimtaka arudie. Naye alirudia.
Mume alitaka kujua ni lini uchafu huu ulikuwa umetendeka. Mke alijibu kama wiki mbili zilizopita. Baba hakupoteza muda. Alimwambia kuwa alikuwa akimdanganya. Na kama kweli alibakwa, kwanini hakuripoti kituo cha polisi? Mama hakuwa na la kujibu bali kukiri kuwa walikuwa wamekubaliana. Mume hakumkawiza. Alimuacha na kuoa haraka sana.
Kufupisha kisa kirefu, je, haya hayapo? Je, ni wangapi wanayajua? Ungekuwa wewe ungefanya nini?
Somo tunalalioona hapa ni kwamba, ni kweli hakuna dawa wala mganga wa mapenzi. Unaweza kutafuta jibu ukidhani unatatua tatizo, kumbe unalikuza.
Kinamama muwe makini na ujinga na upuuzi kama huu. Hakuna cha kuchezewa via vya uzazi bali kuchezewa akili.
