Dar es Salaam. Vile ulivyo leo kama vile haiba yako, tabia zako, na namna unavyojitambua, huundwa na mambo mbalimbali ikiwemo urithi, malezi na makuzi, nafasi yako katika familia, mazingira ya nyumbani, pamoja na marafiki unaochangamana nao.
Mambo haya yote yana mchango mkubwa katika kujenga hulka ya mtu. Hata hivyo, kwa baadhi ya watu, misingi hiyo huacha kumbukumbu mbaya zinazoweza kumtesa mtu kwa muda mrefu na kumzuia kusonga mbele kimaisha.
Ili kuishi kwa furaha na mafanikio, ni muhimu kujifunza kuzifuta au kuzibadili kumbukumbu hizo. Haijalishi ni kwa kiwango gani mabadiliko yanaonekana kuwa magumu, ukweli ni kwamba kila tabia inaweza kubadilika, na fikra zilizoambatana nayo pia zinaweza kubadilika endapo mtu ataamua kwa dhati.
Hatua ya kwanza ni kufahamu kwamba kesho yako haijengwi na jana yako. Maisha ya nyuma yanaweza kuwa na maumivu mengi kama manyanyaso, vipigo, kudharauliwa, kuonewa, aibu, hasara, kusemwa vibaya, au hata kutalikiwa na kushinikizwa.
Licha ya yote hayo, hairuhusiwi kuyaruhusu maisha ya jana yaendelee kuumiza kesho yako. Ingawa yaliyopita yanaweza kuonekana kuathiri hali yako ya sasa, hayapaswi kuwa gereza la maisha yako yajayo. Usibaki kwenye jana; simama, songa mbele na jiambie kwa ujasiri kwamba wewe si yule wa zamani, bali ni mtu aliyekua na anayechagua mwelekeo mpya.
Mabadiliko pia huanza kwa kubadili namna unavyojizungumza na nafsi yako. Jiulize, unajisemeaje? Unajiambia nini kila siku?
Fahamu kuwa una uwezo mkubwa wa kujijenga au kujiharibu kupitia maneno unayojieleza mwenyewe. Hata kama historia yako si ya kupendeza, bado una mamlaka ya kubadili mazungumzo ya ndani ya nafsi yako.
Epuka maneno ya kujidharau, kushindwa au kukata tamaa, kwa sababu mara nyingi kile unachojiambia huanza kuunda uhalisia wako. Maneno mengi hasi tunayojirudia hujengwa tangu utotoni kutokana na tulichoambiwa na watu waliotuzunguka.
Sasa ni wakati wa kuyabadili na kuanza kujisemea maneno ya ushindi, matumaini na nguvu.
Ni muhimu pia kujifunza kuwa mzazi wako mwenyewe. Jilee, jiongoze, jirekebishe na jikaripie pale inapobidi. Jiwazie vile unavyotamani kuwa, kisha chukua hatua ndogo ndogo kuelekea huko. Jifanyie tathmini ya kina na uamue kwa dhati kutaka mabadiliko.
Pale unapofanya vizuri, jipongeze; pale unapohitaji kutiwa moyo, jitie moyo. Jifunze kujisamehe na kujionea huruma. Yote ambayo mzazi mwenye upendo angeweza kumfanyia mtoto wake, jitahidi kuyafanya kwa nafsi yako mwenyewe, kwa sababu yanasaidia sana na huleta matokeo chanya.
Kila mtu amepitia kumbukumbu mbaya katika maisha, lakini tofauti ipo kwenye namna anavyozitumia.
Kuna watu waliopitia historia ngumu sana lakini waliamua kuzitumia kama kichocheo cha mafanikio. Mfikirie Oprah Winfrey, mwanamke mashuhuri aliyepitia maisha ya mateso makubwa lakini akayatumia kama nguvu ya kujijenga.
Mfikirie pia Nelson Mandela, ambaye licha ya historia yenye huzuni na mateso, aliamua kuangalia mbele kuliko kubaki mateka wa yaliyopita.
Wote hawa waligeuza maumivu yao kuwa somo na motisha. Vivyo hivyo, nawe unaweza kujifunza kuzibadili kumbukumbu zako mbaya na kuzitumia kama chanzo cha hamasa.
Usizikimbie wala kuzikwepa kumbukumbu zako; zitafakari, zielewe, kisha zigeuze kuwa daraja la kukuvusha kwenda hatua mpya ya maisha.
Katika safari hii ya uponyaji wa ndani, msamaha ni nguzo muhimu. Wasamehe wazazi wako bila kujali walikuumiza kwa kiasi gani. Msamaha huu si kwa faida yao, bali ni kwa manufaa yako mwenyewe. Kutunza kumbukumbu mbaya ni kama kunywa sumu taratibu; humdhuru anayebeba mzigo huo. Msamaha hukufungua kutoka kwenye gereza la maisha ya nyuma na kukupa nafasi ya kuanza upya. Hausamehi kwa sababu wengine wanahitaji msamaha wako, bali kwa sababu wewe mwenyewe unahitaji uhuru wa ndani.
Mabadiliko ya kweli hayaishii kwenye uamuzi wa akili pekee, bali yanahitaji hatua. Hakuna kinachobadilika bila wewe kufanya kile kinachopaswa kubadilishwa.
Kama mtu ni mgonjwa, hata akitembelea hospitali ngapi au kuwaona madaktari bingwa wangapi, hatapona bila kuamua kutumia dawa na kufuata maelekezo aliyopewa.
Vivyo hivyo, mafunzo na maarifa unayoyapata hayatakuwa na maana kama hutayaweka katika vitendo. Amua sasa kuyatafsiri yote uliyojifunza kuwa hatua halisi katika maisha yako.
Aidha, usiogope kuzungumza na mtu unayemwamini. Wakati mwingine, kubadilika peke yako huwa ni vigumu. Kumbuka kuwa binadamu tunaishi kwa kutegemeana.
Mshirikishe mtu anayekuamini na unayemwamini ili aweze kukusikiliza, kukufuatilia na kukutathmini. Msaada huu huongeza uwajibikaji na hukusaidia kudumisha dhamira ya mabadiliko. Kuomba msaada si udhaifu, bali ni hekima.
Mwisho, kamwe usiamini uongo unaotoka kwenye kumbukumbu zako za maisha ya awali. Acha kujidanganya kwa sauti za ndani zinazokurudisha nyuma.
Amka, ifuate kesho yako. Amka, ifuate ndoto yako. Inawezekana, na uwezo huo upo ndani yako.
