WAFANYABIASHARA 500 WAPATIWA MAFUNZO YA UNUNUZI WA UMMA DAR

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simbaali  Akizungumza wakati wa mafunzo maalum ya ununuzi wa umma yaliyoendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

:::::::::::

Wafanyabiashara wapatao 500 jijini Dar es Salaam wameshiriki mafunzo maalum ya ununuzi wa umma yaliyoendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuwawezesha wazawa kushiriki kikamilifu katika zabuni za miradi ya umma.

Kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023, Serikali imeweka upendeleo maalum kwa wazabuni wa ndani kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, amesema miradi yote ya serikali yenye thamani ya hadi shilingi bilioni 50 inapaswa kutekelezwa na wazabuni wa ndani.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simbaali Akizungumza wakati wa mafunzo maalum ya ununuzi wa umma yaliyoendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Ametoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa hiyo ipasavyo kwa kufuata sheria na viwango vilivyowekwa.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Kenneth Ndebuka, amesema mifumo ya ununuzi wa umma inaendeshwa kwa uwazi na uajibikaji.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewasaidia kuelewa kwa undani namna ya kushiriki zabuni za serikali kwa njia sahihi.

Wamesema mafunzo hayo pia yamewasaidia kuepuka makosa yanayoweza kuwanyima fursa za kushiriki katika zabuni za umma.

Naye Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Huduma za Sheria wa PPAA, Bi. Florida Mapunda, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wadau wa ununuzi wa umma kuhusu matumizi ya moduli ya usimamizi wa malalamiko na rufaa kielektroniki.

Amesema moduli hiyo inatumika kupitia mfumo wa NeST katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza.

Bi. Mapunda amesema kwa sasa Sheria ya Ununuzi wa Umma imeweka sharti la lazima kwa ununuzi wa umma kufanyika kwa njia ya kielektroniki kupitia mfumo wa NeST.

Kutokana na sharti hilo, amesema PPAA kwa kushirikiana na PPRA wamejenga moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo huo.

Ameeleza kuwa moduli hiyo inawasaidia wadau wa ununuzi kuwasilisha malalamiko na rufaa kielektroniki.

Bi. Mapunda ameongeza kuwa moduli imerahisisha uwasilishaji wa malalamiko yatokanayo na michakato ya ununuzi wa umma.

Amesema pia imesaidia utunzaji wa kumbukumbu za taarifa za malalamiko na rufaa zinazowasilishwa katika michakato yote ya ununuzi wa umma.

Mafunzo hayo ya siku moja kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST yamefanyika Januari 10, 2026 katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya.

Lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kutoa elimu kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma nchini.