Maswa. Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa) mkoani Simiyu imetakiwa kukamata watu wanaoingiza mifugo katika Bwawa la New Sola lililopo Kijiji cha Zanzui wilayani humo.
Maelekezo hayo yametolewa leo Januari 11, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney kufuatia kuongezeka kwa wimbi la wafugaji wanaoingiza mifugo katika bwawa hilo, ambalo ndilo chanzo kikuu cha maji kinachotegemewa na wakazi wa Mji wa Maswa pamoja na vijiji 12 vinavyohudumiwa na Mauwasa.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney akizungunza na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo (hawako pichani) juu ya ulinzi wa Bwawa la New Sola .Picha na Samwel Mwanga
Dk Anney amesema kuna sheria mbalimbali zinazolinda vyanzo vya maji, mazingira pamoja na sheria za mifugo, hivyo hakuna mtu aliye juu ya sheria hizo.
“Bwawa la New Sola ndilo chanzo cha maji tunayotumia sisi wananchi wote wa Maswa. Bila bwawa hili hakuna maisha, maana hatutapata maji. Sheria zipo wazi kulinda vyanzo vya maji na mazingira na lazima isimamiwe,” amesema.
Ameeleza kuwa, katika maeneo ya bwawa hilo wapo viongozi wa Serikali kuanzia mtendaji wa kijiji, kata na Mauwasa, lakini bado wafugaji wanaendelea kuingiza mifugo kwenye hifadhi ya bwawa hilo kinyume cha sheria.
“Haiwezekani hali hii iendelee. Nendeni mkakamate watu wote wanaoingiza mifugo kwenye bwawa, na wawajibishwe kwa mujibu wa sheria. Pia, wale waliolima ndani ya hifadhi ya bwawa wasivune mazao yao. Tukichezea bwawa hili, litapotea na tutakosa maji,” amesisitiza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias amesema changamoto kubwa kwa sasa ni wafugaji kuingiza mifugo ndani ya bwawa kwa ajili ya kunywesha maji, licha ya kuwepo kwa mabirika maalumu ya kunyweshea mifugo yaliyojengwa nje ya hifadhi ya bwawa.
Amesema kitendo hicho kinahatarisha uhai wa bwawa na ubora wa maji yanayotumika kwa matumizi ya binadamu.
Mkurugenzi Mtendaji Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias (Kulia) akieleza jinsi wafugaji wanavyoingiza mifugo katika Bwawa la New Sola . Picha na Samwel Mwanga
“Uingizaji wa mifugo katika Bwawa la New Sola unasababisha uchafuzi wa maji kwa njia ya kibaiolojia, hupunguza ufanisi wa matibabu ya maji na kuongeza gharama za uendeshaji. Hali hii, kama haitadhibitiwa mapema, inaweza kusababisha uhaba mkubwa wa maji mjini Maswa,” amesema.
Aloyce Shimbi ni mkazi wa mjini Maswa ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatari ya kupotea kwa chanzo hicho cha maji huku akitaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wanaokiuka sheria.
“Maji haya tunakunywa sisi na watoto wetu. Ukiona ng’ombe wanakunywa na kukanyaga ndani ya bwawa, unajiuliza usalama wa afya zetu uko wapi. Serikali isimamie sheria bila muhali,” amesema.
Rehema Masanja, mkazi wa Kijiji cha Zanzui wilayani humo amesema baadhi ya wafugaji wamekuwa wakikaidi makusudi maagizo ya Serikali.
“Tunawaona kila siku, hata wakikatazwa wanaendelea. Kama hawatachukuliwa hatua kali, bwawa litaendelea kuharibika na sisi wananchi wa kawaida tutapata mateso ya uhaba wa maji,” amesema.
Naye Slivester Lugembe,mkazi wa mjini Maswa amesema ni vizuri kwa Mauwasa kushirikiana na viongozi wa vijiji, kata vinavyolizunguka bwawa hilo pamoja na vyombo vya dola kufanya doria za mara kwa mara ili kulinda chanzo hicho muhimu cha maji.
“Bwawa la New Sola ni mhimili mkuu wa huduma ya majisafi na salama mjini Maswa, hivyo ulinzi wake ni suala la uhai na maendeleo ya wakazi wa wilaya ,i vizuri kwa Serikali kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kuhatarisha chanzo hicho cha maji,” amesema.

