WANANCHI WAMPA MBUZI DUME MBUNGE MAGEMBE

………..

CHATO

WANANCHI wa kata ya Kasenga wilayani Chato mkoani Geita, wamemtunuku zawadi ya mbuzi dume Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Mwl. Cornel Magembe, baada ya kuwaondolea adha ya usafiri iliyokuwa ikiwakabili kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.

Wamesema hivi sasa wanafurahia uwepo wa barabara nzuri katika maeneo yao baada ya serikali kufungua mtandao wa barabara ndani ya Jimbo hilo.

Kutokana na hali hiyo, wamelazimika kuonyesha shukrani zao kwa Mbunge huyo baada ya kutimiza ahadi yake aliyoitoa kipindi cha kampeni za Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani 2025, kuwa wananchi watakuwa na uhakika wa usafiri kutoka kata ya Kasenga hadi Mwanza.

Hata hivyo, John Gayamahyo,mkazi wa Kijiji cha Kihula amemuomba Mbunge huyo, kuendelea kufungua barabara zingine za kata hiyo ili kusaidia wakulima kusafirisha mazao yao kutoka mashambani.

Hatua hiyo itasaidia kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja, Kaya na Taifa kwa ujumla na kwamba wanajivunia kuwa na uwakilishi wenye kutatua changamoto zao.

Kadhalika Bahati Jason, akakumbushia ahadi ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya ujenzi wa barabara ya lami ya kutoka Nyamirembe hadi Katoke wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Akijibu changamoto za wananchi, Magembe amewahakikishia kuwa barabara ya Nyamirembe hadi Katoke yenye urefu wa km 50 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami baada ya serikali kumthibitishia kwa kutenga fedha.

Magembe amesema changamoto mbalimbali za wananchi hao zitaendelea kutatuliwa kulingana na vipaumbele na kwamba zipo zitakazofanyiwa kazi na halmashauri ya wilaya, serikali kuu,wadau wa maendeleo na hata jamii yenyewe.

Baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na wananchi ni pamoja na uhaba wa maji safi na salama, barabara, Zahanati, vyumba vya madarasa, michezo, usafiri wa anga kupitia uwanja wa ndege wa Geita uliopo Chato pamoja na mahusiano ya watumishi wa hifadhi ya taifa ya Burigi – Chato dhidi ya wananchi.

Hata hivyo Mbunge huyo amesema ziara yake kwa wananchi hao ni kuchukua kero zao na kuziwasilisha Bungeni kwaajili ya utekelezaji badala ya kupeleka mawazo yake binafsi, huku akitoa ahadi ya madawati 120 kwa shule za msingi sita zilizopo kwenye kata hiyo.

                              Mwisho.