Wanne wafariki dunia ajalini Tanga, 16 wajeruhiwa

Korogwe. Ajali nyingine ya gari imetokea katika Mkoa wa Tanga na kusababisha vifo vya watu wanne huku wengine 16 wakijeruhiwa.

Ajali hiyo ni ya tatu iliyosababisha vifo ndani ya siku chache za mwanzo wa mwaka 2026 na mwishoni mwa 2025.

Ajali ya kwanza ilitokea Morogoro, Desemba 31, ikiua watu 10 na kuwajeruhi 18.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo, Jumapili Januari 11, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, inaeleza kuwa, ajali hiyo imehusisha magari mawili kugongana uso kwa uso, saa 9:30 asubuhi katika eneo la Mkumbara, Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe, kwenye barabara kuu ya Same–Korogwe.

Inaeleza kuwa, ajali hiyo imehusisha gari la mizigo aina ya Scania likiwa na tela mali ya Kampuni ya Mikoani Edible Oil and Detergents Ltd, lililokuwa likitokea Same kuelekea Korogwe- Tanga na basi aina ya Yutong mali ya Kampuni ya Mwensino, lililokuwa likitokea Lushoto kuelekea mkoani Arusha.

“Kutokana na ajali hiyo, watu wanne wamepoteza maisha, wakiwamo Hazhadir Iddy maarufu Mohamed (30), Msambaa, fundi wa magari na mkazi wa Goha wilayani Lushoto na wanaume wengine watatu ambao majina na umri wao bado haujatambuliwa,” inaeleza taarifa hiyo.

Aidha, inaeleza kuwa, watu 16 wamejeruhiwa katika ajali hiyo, wakiwamo madereva wa vyombo hivyo na abiria na kwamba majeruhi wote wamepelekwa katika Kituo cha Afya Mombo na wanaendelea kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la mizigo aina ya Scania kushindwa kulimudu, hali iliyosababisha kuvuka kutoka upande wake wa kushoto na kuingia upande wa kulia wa barabara, kisha kugongana uso kwa uso na basi hilo.

“Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Mombo kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria na uchunguzi zaidi,” inaeleza taarifa hiyo.

Jeshi hilo, limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka mwendokasi, uzembe na kufanya uamuzi hatarishi wanapokuwa barabarani.