Watoa angalizo waliofeli kidato cha pili kuendelea kidato cha tatu

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kueleza wanafunzi waliofeli mitihani yao ya kidato cha pili badala ya kurudia darasa, watafanyiwa programu maalumu huku wakiendelea na kidato cha tatu, wadau wa elimu nchini wametoa angalizo.

Januari 10, 2026 Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa katika taarifa yake aliyoitoa kwa umma alisema waliofeli watapewa programu maalumu rekebishi (remedial programme) itakayotolewa wakati wakiendelea na masomo yao ya kidato cha tatu.

Kamishna huyo alieleza uamuzi huo unazingatia mitaala iliyoboreshwa inatekelezwa kwa awamu na wanafunzi waliofanya upimaji wa kidato cha pili mwaka 2025, waliotumia mtaala wa zamani na watamaliza kidato cha nne kwa kutumia mtaala huo huo.

“Wanafunzi wanaoingia kidato cha pili mwaka 2026 watatumia mtaala ulioboreshwa ambao walianza kuutumia kidato cha kwanza, hivyo endapo   walioshindwa kufikia alama za ufaulu watarudia kidato cha pili mwaka 2026, watalazimika kutumia mtaala ulioboreshwa ambao hawakuanza nao kidato cha kwanza. Hii italeta changamoto kubwa katika ujifunzaji na ufundishaji,” alifafanua zaidi.

Wakiichambua hoja hiyo, baadhi ya wadau wa elimu waliozungumza na Mwananchi leo Jumapili, Januari 11, 2025 wamesema ni sahihi licha ya kutoa angalizo wakishauri ufanyike kwanza utafiti wa sababu za kushindwa kufikia alama za ufaulu kabla ya kuanzishiwa programu hiyo maalumu.

Mdau wa elimu, Richard Temu amesema kwa hoja iliyotolewa na Serikali, hakuna namna zaidi ya waliofeli kusonga mbele.

“Hata hivyo, katika hili kuna mambo mawili ya kuangaliwa, hawa waliofeli wanapochanganywa na wengine, kisaikolojia itawavuruga, kama Serikali ingeweza kuwapa eneo moja la wao kukutanikia na kuendelea na masomo.

“Lakini pia kabla ya kuwapa programu maalumu wafanyiwe tathimini, sababu gani imesababisha wafeli je, ni kutojua kusoma na kuandika? ambayo ni changamoto kubwa.

“Au hawakuwa na mwalimu, au hawakumaliza topic (mada) na sababu nyinginezo, kwani bila kufanya tathimini ni sehemu zipi wamefeli hawataweza kuwasaidia, itakuwa ni kama kutoa dawa moja kwa wagonjwa tofauti,” amesema.

Mdau mwingine, Dk Muhanyi Nkoronko amesema si ajabu ikatokea katika programu hiyo maalumu, wengine wakajikuta wakipotezwa na kuachwa njiani, huku akishauri ufanyike utafiti kujua chanzo cha wao kufeli.

Dk Nkoronko ambaye pia ni mtafiti wa elimu amesema unahitajika utafiti kufahamu chanzo cha wao kufeli kabla ya kuwaanzishia programu maalumu.

Amesema kunahitajika juhudi za makusudi kuwa na programu ambayo itamtengeneza huyo mwanafunzi aliyefeli kwa miezi kadhaa wakati huo huo, wakijifunza mtaala mpya ili waendelee kujengwa katika mahiri za zamani ili isije kutokea wengine wakapotezwa kabisa,” amesema.

Mbali na angalizo kwa wanafunzi waliofeli kidato cha pili, wadau hao pia wametaja suluhisho la wanafunzi wanaoandika lugha za matusi kwenye mitihani yao.

Jana akitangaza Januari 10, 2026, akitangaza matokeo ya mitihani ya upimaji ya kidato cha pili na darasa la nne, Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohammed alisema wanafunzi 19 waliandika lugha za matusi.

Huo ni mwendelezo wa baadhi ya wanafunzi kujaza matusi ambapo kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka jana, wanafunzi watano waliandika lugha ya matusi kwenye mitihani yao.

Ili kukomesha tatizo hilo, wadau wa elimu wameshauri itumike njia rafiki ya kufahamu sababu za wanafunzi kuendelea kujaza lugha za matusi kwenye mitihani.

Richard amesema kama wanafunzi hao wameweza kuandika matusi, basi ni dhahiri wanaweza kuandika masomo waliyofundishwa.

“Ingekuwa hawajui kuandika wangechorachora, lakini wameweza kuandika, hii huenda inaashiria kuna hali hawakubaliani nayo.

“Ili kubaini ni nini? haihitaji kutumia dola au adhabu, bali ni kufuatilia kwa upendo kubaini nini kimewasukuma kuandika hivyo,” amesema.

Amesema wengine huenda ni matatizo ya saikolojia, akifafanua kwamba wanafunzi wa aina hiyo hawana tofauti na wale wanaoambiwa na wazazi wao wasifaulu makusudi.

“Yawezekana hilo likawa ni moja ya tatizo, tufuatilie kujua ni kwa nini wanaandika hivyo, ni taarifa gani huyo mtoto anajaribu kuiwasilisha kwa jamii na kwa msahishaji wa mtihani bila kutumia adhabu,” amesema.

Dk Nkoronko kwa upande wake amesema kuna mambo matatu ya kuweza kutatua changamoto ya baadhi ya wanafunzi kujaza matusi kwenye mitihani yao.

“Kwanza ni kushirikiana kwa wazazi, walimu na jamii kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili, jambo la pili ni kufundisha kwa hakika ili mwanafunzi akitoka darasa moja kwenda jingine basi awe amepata mahiri stahiki,” amesema.

Amesema kunahitajika ufuatiliaji katika kuhakikisha mwanafunzi amepata mahiri za kumjenga kabla ya kuingia darasa jingine.

“Jambo la tatu ni kuhakikisha wanahudhuria vipindi kama inavyotakikana, wengi wanaoandika matusi ni wale ambao hata mahudhurio yao shuleni ni hafifu, hii inasababisha kushuka kwa value (thamani) ya elimu, kwa kuwa wapo wanaokwenda shuleni kwa kulazimishwa,” amesema.