Arusha. Zikiwa zimesalia siku chache Shule za Msingi na Sekondari kufunguliwa nchini, wazazi na walezi nchini wametakiwa kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanaripoti na kuanza masomo.
Wametakiwa kutambua kuwa kusomesha watoto ni hazina wameweka na kusaidia kuongeza mabadiliko katika jamii.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-Utumishi, Regina Qwaray, amesema hayo leo Jumapili Januari 11, 2026 ametoa maagizo hayo wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari ya Laja, iliyopo wilayani Karatu Mkoa wa Arusha.
“Wazazi na walezi mnapaswa kutambua ukisomesha watoto umeweka hazina na vijana wetu wakakaposoma watakuja kutusaidia sisi, elimu inafungua mtu akili na ukishakuwa na wasomi wengi tegemea mabadiliko,” amesema. “Nitoe wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye umri wa kwenda shule wahakikishe wameenda na hata waliofaulu darasa la saba, tusiwaache mtaani tuendelee kuhakikisha wanapomaliza darasa la saba wanaendelea na kidato cha kwanza.”
Akizungumzia shule hiyo ambayo imejengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kupitia mradi wa Opec, amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa kipaumbele hasa katika miradi ya elimu ili kuondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule.
“Kupitia mradi huu tunaona wanafunzi kwa sasa wanasoma karibu, kuna mabweni na niwapongeze wananchi kwa kujitoa kwenu na kuona thamani ya elimu ,”
“Tuhakikishe mradi unatunzwa kwa wivu mkubwa kwani tusipotunza tutaingia gharama kubwa, tunaona manufaa ya mradi kama huu ni wanafunzi wa kike kuondokana na changamoto ya ndoa za utotoni na wengine kujiingiza kwenye vitendo viovu.”
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Juma Hokororo, ameshukuru Tasaf kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu ambayo imesaidia kwa kiwango kikubwa kuinua elimu na miundombinu mbalimbali katika shule.
Amesema halmashauri hiyo imeweka mkakati kuhakikisha watoto wote ambao wana umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kuripoti.
“Katika kipindi shule zinapokaribia kufunguliwa halmashauri tumeshaweka mkakati kuhakikisha watoto wote ambao wana umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kuripoti shule,” amesema
“Rai yangu kwa wazazi ni kuhakikisha watoto wanakwenda shuleni kwani Serikali imesema kusiwe na kikwazo cha wanafunzi kwenda shule, sare za shule isiwe kikwazo cha kusababisha mtoto asiende shule,”
Kaimu Mratibu wa Tasaf wilaya ya Karatu, Athanasi Sarwatt, amesema mradi huo wa shule umegharimu Sh774.9 milioni ambapo Tasaf imetoa Sh659.5 milioni na zaidi ya Sh115milioni zikiwa ni michango ya wananchi ikiwemo mchanga, kokoto, maji, mawe na nguvu kazi.
Amesema mradi huo umepunguza utoro kwa wanafunzi kwani wengi walikuwa wakitembea umbali mrefu hadi kilomita nane kwenda shule na kuwa mradi umesaidia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi hususani wanaotoka kaya maskini.
