Aliyeitungua Simba, aibukia Singida Black Stars

KLABU ya Singida Black Stars, imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Fufuni ya Pemba, Mboni Stephen Kibamba ambaye aliitungua Simba katika mechi ya makundi katika Kombe la Mapinduzi 2026.

Mshambuliaji huyo ambaye ni kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Zanzibar msimu huu akihusika na mabao 16 katika mechi 15, akifunga 10 na asisti sita, anatua Singida baada ya klabu hiyo kuvutiwa na uwezo wake.

Taarifa kutoka ndani ya kambi ya Singida iliyoiweka kisiwani Unguja wakati inashiriki Kombe la Mapinduzi 2026 na kutolewa nusu fainali, zinasema mshambuliaji huyo mwenye hat-trick moja msimu huu amesaini mkataba wa miaka mitatu.

“Tumempa mkataba wa miaka mitatu, hii ni sehemu ya maboresho ya kikosi chetu eneo la mbele na tunaamini atatusaidia kutokana na uwezo wake wa kufunga na kutengeneza nafasi,” kimesema chanzo hicho.

Hivi karibuni, Mboni alipofanya mahojiano na Mwanaspoti, alionyesha matamanio yake ya kucheza Ligi Kuu Bara akisema: “Timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ikinifuata nitasaini kwa sababu natamani kutafuta changamoto nyingine.”

Kabla ya kutua Singida, Mboni alikuwa akihusishwa na Coastal Union ambayo ilikuwa ya kwanza kumuhitaji.