Alliance Girls yajipanga kubakiza pointi nyumbani

KOCHA wa Alliance Girls, Sultan Juma amesema kikosi hicho kimeweka mikakati ya kuhakikisha kinabakiza pointi tatu katika michezo yote ya nyumbani watakaocheza Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kufanya vizuri katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Wanawake.

Msimu uliopita Alliance Girls ilimaliza ligi katika nafasi ya nane, ikiwa na pointi sawa na Baobab Queens walioteremka daraja sambamba na Geita Gold Queens, tofauti ikiwa ni idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Akizungumza na Mwanaspoti Juma amesema msimu uliopita walijikita zaidi katika kujenga timu, msimu huu malengo yao ni kuhakikisha wanakaa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, licha ya ushindani mkubwa uliopo.

“Ligi ni ngumu, timu zimejiimarisha, lakini sisi tumejipanga kuhakikisha tunatumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani kwa kubakiza pointi zote tatu,” amesema Juma

Aliongeza, licha ya kuwatumia wachezaji wengi wachanga lakini kwa kiasi kikubwa wameonyesha upinzani kwa timu kubwa akikiri hilo limeongeza morali hasa wanacheza nyumbani.

“Tunajua bado tuna safari ndefu, lakini mwanzo huu unatupa matumaini makubwa, karibu kikosi kizima kina wachezaji wachanga wakipata uzoefu kidogo nafikiri tutakuwa na timu nzuri baadae.”

Msimu huu Alliance imeanza na mabadiliko makubwa hususani kwenye mechi za nyumbani na tayari ikifanikiwa kupata ushindi katika mechi zote tatu ilizocheza.

Alliance Girls iliitandika Geita Gold Queens mabao 2-1, ikaifunga Fountain Gate Princess bao 1-0, na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ceasiaa Queens.

Kwenye mechi saba ilizocheza Alliance imeshinda nne ikipoteza tatu za ugenini.