Bei ya viazi yapaa, kamati ya Serikali ikiendelea na uchunguzi

Mbeya. Wakati timu ya wataalamu 11 iliyoundwa na Serikali jijini Mbeya ikiendelea na uchunguzi juu ya kupanda kwa bei ya bidhaa, hali imeendelea kuwa tete kufuatia viazi mviringo kupaa kufikia hadi Sh20,000 kwa ndoo ya lita 20.

Pamoja na kupaa kwake, bado wafanyabiashara wameeleza kuwa huenda bei ikaendelea kupaa kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo ikilinganishwa na uhitaji wake sokoni.

Awali, Desemba 2025  bei ya bidhaa hiyo ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh9,000 hadi Sh11,000 kulingana na mazingira na ubora wa chakula hicho, lakini kwa sasa imeongezeka zaidi ya mara mbili yake na kushtua wananchi.

Januari 2 mwaka huu, kamati ya ulinzi na usalama wilayani Mbeya chini ya mkuu wa wilaya hiyo, Solomon Itunda ilifanya ziara ya kushtukiza katika Soko la Mwanjelwa kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya bidhaa jijini humo.

Baada ya ziara hiyo, Itunda alitangaza timu ya wataalamu 11 watakaofanya uchunguzi wa kupanda kwa bei hiyo, akieleza kuwa, baada ya siku tatu itawasilisha ripoti ili kufanyiwa kazi na bei kurejea katika hali ya kawaida.

Hatua hiyo ilifikiwa ikiwa ni baada ya siku moja Gazeti la Mwananchi kuripoti bei ya vitu kupaa ikiwa ni mchele uliofika hadi Sh70,000 kwa ndoo ya kilo 20, sukari kuuzwa Sh4,000 badala ya Sh3000 na sabuni ikifika Sh4,200.

Hata hivyo, leo Januari 12, Gazeti hili limefika katika Soko la Soweto na kushuhudia bei ya viazi mviringo ikifika Sh20,000 badala ya Sh11,000 iliyokuwapo awali, huku sababu kadhaa zikitajwa kupaisha bidhaa hiyo muhimu.

Mbali na viazi, nyanya nazo hali imebadilika kwa kuuzwa Sh8000 kwa sado moja badala ya Sh5000 iliyokuwapo Desemba hali inayoleta sintofahamu kwa wananchi.

Mfanyabiashara Magreti Charles amesema kupanda kwa bei hiyo ni kutokana na uhaba wake shambani baada ya mvua kukosekana na kusababisha kupungua kwa uzalishaji ikilinganishwa na mahitaji yenyewe.

Amesema kadri siku zinavyokwenda, bei huenda ikaongezeka kwakuwa malori yamepangana shambani wakishindanisha bei, akieleza kuwa wananchi wawe wavumilivu kwa kipindi hiki.

“Gunia la debe sita liliuzwa Sh50,000 na hata Sh40,000 ingewezekana kuchukua lakini kwa sasa tunachukua  kwa Sh110,000 hadi Sh120,000, uzalishaji umepungua mvua zilikuwa chache.

“Kwa kinachoendelea shambani huenda bei ikaendelea kupanda kwakuwa kuna magari yale makubwa kutoka mikoani wanashindana bei, kwa hiyo sisi tunanunua kiasi kidogo hali itakuwa ngumu,” amesema Magreth.

Yusuf Daud amesema kupanda kwa bei hiyo ni kutokana na mabadiliko ya kawaida katika maisha ya binadamu kwani hata kilimo kwa sasa ni gharama kubwa inatumika kuanzia maandalizi hadi mavuno.

“Mfano nyanya kwa sasa ni kama msimu, lakini zile mvua zilizofululiza ziliharibu uzalishaji kwakuwa dawa iliyopulizwa haikuwa na faida kwakuwa ilipukutishwa.

“Suala la viazi ni kama mazao mengine kwa sababu kuanzia maandalizi ya mahitaji gharama, kukodi shamba, mbolea, vibarua na usafirishaji lazima hali ya tofauti iwepo,” amesema Daud.

Mmoja wa wananchi, Exavery Ntungwa amesema kwa sasa ni kufunga mkanda kutokana na vitu vingi kupanda bei akieleza kuwa, Januari imeanza kwa ugumu kwa kuwa kila sehemu inahitaji gharama.

“Ni kujifunga mkanda, tuna watoto wanafungua kesho shule wanataka ada na matumizi ya shuleni, vyakula bei ndio kama unavyoona, sijui kodi za nyumba napo wanadai, tutafika ila… ” Amesema Ntungwa mjasiriamali wa vifaa vya urembo stendi ya Kabwe.

Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda kuhusu matokeo ya timu ya wataalamu iliyoundwa kuchunguza kupanda kwa bidhaa, amesema bado inaendelea na kazi yake na ikikamilisha, wataweka wazi msimamo.