DC KASILDA AWATAKA WAHANDISI KUTOKA MAOFISINI

NA WILLIUM PAUL, SAME. 

MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amewataka wahandisi wa Halmashauri kuacha tabia ya kukaa ofisini na badala yake kushuka moja kwa moja kwenye miradi ya kimaendeleo, akisisitiza kuwaacha walimu wakuu wa shule na mafundi peke yao kusimamia na kujenga ni hatari kwa ubora wa ujenzi wa miradi na husababisha miradi kujengwa chini ya viwango.

Kasilda ameyasema hayo jana wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu katika Shule ya Msingi Hedaru.

Alisisitiza kuwa ni wajibu wa wahandisi wa ujenzi kushiriki kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi ili kuepusha kasoro zinazoweza kujitokeza endapo mafundi na kamati za ujenzi wataachwa kufanya kazi bila usimamizi wa karibu wa wataalam.

“Niwasisitize sana wahandisi wa ujenzi wa Halmashauri kuhakikisha mnafika kwenye miradi inayotekelezwa mara kwa mara, msiwaachie mafundi na kamati za ujenzi peke yao, tunahitaji kila hatua ya ujenzi isimamiwe na wataalam, kwa kushirikiana na TAKUKURU, ili ushauri na marekebisho yafanyike mapema kabla mradi haujafikia hatua kubwa zaidi,” alisema Kasilda.