KIPA wa zamani wa Yanga anayekipiga kwa sasa Mashujaa akiwa ndiye kinara wa ‘cleansheet’ katika Ligi Kuu Bara, Erick Johola amesema ubora alionao unatokana na mambo manne ikiwamo kujiamini, kupambana, nidhamu na kuonyesha kila unapopewa nafasi na kuaminiwa na benchi la ufundi.
Kipa huyo anaongoza ya makipa waliokomaa mechi nyingi bila kuruhusu bao akiwa na clean sheets sita katika mechi saba alizodaka, akifuatiwa na Constantine Malimi wa Mtibwa Sugar na Omary Gonzo (JKT Tanzania) walio na nne kila mmoja.
Johola aliyefanikiwa kushinda vita ya namba mbele ya makipa wenzake, Patrick Muntari na Lameck Kanyonga, akiwa ameanza katika mechi saba kati ya tisa ilizocheza Mashujaa iliyopo nafasi nne ikiwa na pointi 13 kutokana na mechi tisa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Johola amesema siri kubwa ya mafanikio hayo ni kufuata maelekezo ya kocha na kujituma na kuongeza ubunifu.
“Ni kupambana tu kila ninapopata nafasi ya kucheza. Tunaamini katika kupambana lazima ufuate kile mwalimu anachokuelekeza, kuongezea kile ulichonacho na kujituma ndio maana mpaka sasa hivi mambo ni mazuri,” amesema Johola, kipa wa zamani wa Aigles Noir ya Burundi kabla ya kusajiliwa Yanga.
Amesema pamoja na kujituma pia aliamini kila kitu kinawezekana licha ya ushindani wa namba uliopo katika eneo lake, huku akiamini safari bado ni ndefu.
“Nimecheza mechi saba kati ya tisa za timu yetu ila bado sijafikia malengo, bado inatakiwa nipambane sana ili kufikia malengo niliyojewekea msimu huu,” amesisitiza Johola.
