Kali nne za Mapinduzi Cup 2026

KESHO Jumanne, ile safari ya takribani siku 17 katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inakwenda kuhitimishwa kwa kupigwa mechi ya fainali.

Ni mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa pale Azam itakapocheza dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Mechi hii inazikutanisha timu mbili ambazo kila moja ina sifa yake. Azam ni bingwa wa kihistoria wa Kombe la Mapinduzi ililibeba mara tano zikiwa ni nyingi kuliko timu yoyote, wakati Yanga nayo ni bingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara ikibeba taji mara 31.

Timu hizo zinafahamiana vizuri kwani mara kadhaa zimekuwa zikikutana katika michuano mingine ya ndani ikiwamo Ligi Kuu Bara ambapo kwa msimu huu, hii itakuwa mara ya kwanza kukutana.

Kwa sasa maandalizi ya mechi ya fainali yanakwenda vizuri na hadi kufikia sasa, michuano hii imepitia nyakati mbalimbali za furaha na huzuni ambapo hapa kuna matukio manne tunakuchambulia uyafahamu kabla ya kesho hujashuhudia fainali.

MAPI 03

Kati ya timu 10 zilizoshiriki Kombe la Mapinduzi, hadi kufikia sasa ni Yanga pekee ambayo haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.

Yanga iliyocheza mechi tatu zikiwamo mbili hatua ya makundi na moja nusu fainali, imefunga mabao matano na kulinda vizuri lango lake lisiguswe.

Katika mechi hizo zote tatu, Aboutwalib Mshery ndiye amedaka, na kumfanya kuwa kipa mwenye clean sheet nyingi ambazo ni tatu, akifuatiwa na Aishi Manula wa Azam mwenye mbili akicheza mechi nne.

MAPI 02

Katika mashindano ya mwaka huu kuna Tuzo ya Fair Play ambapo hatua ya makundi mchezaji mwenye kuonyesha mchezo wa kiungwana alikabidhiwa Sh500,000 na nusu fainali ikawa Sh1 milioni, huku fainali ikipanda hadi Sh2 milioni.

Tulishuhudia hatua ya makundi zikitoka kadi za njano tu, lakini nusu fainali, ikachafuka zaidi, kadi nyekundu tatu zimeonyeshwa katika mechi mbili.

Beki wa Simba, David Kameta ‘Duchu’, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika michuano hiyo kuonyeshwa kadi nyekundu msimu huu ambapo tukio hilo lilitokea katika hatua ya nusu fainali, Simba ikifungwa 1-0 na Azam, Januari 8, 2026.

Duchu kwanza alionyeshwa kadi ya njano katika dakika ya 58 kwa kumuangusha Cheikna Diakite, kisha dakika ya 90+2 akaonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu kwa kosa la kusukumana na mwamuzi Mohamed Simba akipinga uamuzi wake.

Siku iliyofuatia, Januari 9, 2026, zilionyeshwa kadi mbili nyekundu na kufanya idadi kufika tatu.

Walioonyeshwa kadi hizo ni Mohamed Damaro wa Yanga na Morice Chukwu wa Singida Black Stars.

Damaro alionyeshwa kadi hiyo baada ya kumchezea rafu Chukwu ambaye naye aliadhibiwa kwa kadi hiyo kutokana na kuonekana akirudisha mashambulizi.

Tukio hilo lilitokea dakika ya 85, ambapo katika kuwania mpira wa juu, Damaro alionekana kumpiga kiwiko Chukwu ambaye baada ya kuanguka, akaamka haraka na kwenda kumsukuma mwenzake. Mwamuzi Rashid Farahan akaanza kumuonyesha kadi ya njano Damaro ambayo ilikuwa ya pili baada ya kwanza kuonyeshwa dakika ya 33, hivyo ikafuatia nyekundu, huku Chukwu akionyeshwa nyekundu moja kwa moja.

MAPI 04

Kiungo huyu wa Simba mwenye uwezo wa kucheza pia safu nzima ya ulinzi, ndiye mchezaji pekee hadi sasa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, aliyebeba tuzo mbili tofauti zinazotolewa.

Nyota huyo raia wa Guinea, alianza kubeba Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi, kisha akabeba Tuzo ya Mchezaji Mwenye Mchezo wa Kiungwana ‘Fair Play’.

Januari 5, 2026 wakati Simba ikishinda 2-1 dhidi ya Fufuni na kufuzu nusu fainali, alitunukiwa Tuzo ya Mchezaji Bora iliyokwenda sambamba na kiasi cha Sh1 milioni.

Baada ya hapo, Januari 8, 2026, Simba ilipochapwa 1-0 na Azam hatua ya nusu fainali na kutupwa nje ya mashindano, ndipo Camara akapewa Tuzo ya Fair Play na Sh1 milioni.

Wakati Camara akibeba tuzo zote za mashindano hatua ya makundi na nusu fainali, Morice Chukwu anazo tuzo mbili za Mchezaji Bora alizoshinda hatua ya makundi, huku Yakoub Said Mohamed wa Muembe Makumbi akibeba tuzo mbili za Fair Play kama ilivyo kwa beki wa Singida, Abdulmalick Zakaria aliyebeba hatua ya makundi na nusu fainali.

Maxi Nzengeli wa Yanga naye ana tuzo mbili za mchezaji bora, akibeba hatua ya makundi na nusu fainali.

MAPI 01

MABAO 28, BALAA LIPO HAPA

Katika mechi 14 zilizochezwa kuanzia makundi hadi nusu fainali, jumla ya mabao 28 yamepatikana. Kati ya hayo, mawili ni ya kujifunga kutoka kwa beki wa KVZ, Rahim Andrea.

Wakati yakipatikana mabao hayo, balaa lipo kipindi cha pili kwani ndiyo yamefungwa mengi yakifika 17, huku cha kwanza yakipatikana 11.

Wanaoongoza kwa mabao ni Joseph Guede wa Singida, Idrissa Diomande (Singida BS), Mboni Stephen Kibamba (Fufuni) na Jephte Kitambala (Azam) kila mmoja akiwa nayo mawili.

Cha kufurahisha zaidi, hakuna mechi iliyomalizika bila bao, zote tumeshuhudia nyavu zikitikiswa.