Kiungo kiraka ajipa kazi Geita Gold

KIUNGO mpya kiraka wa Geita Gold, Raymond Masota amesema ujio wake ndani ya timu hiyo unaiongezea nguvu katika mapambano ya kupanda daraja kwenda Ligi Kuu Bara, huku akiahidi kuisaidia ili lengo hilo litimie.

Masota anayemudu kucheza nafasi ya winga, kiungo mshambuliaji na beki wa kulia, alijiunga na Geita Gold Januari 8, mwaka huu katika usajili wa dirisha dogo akitokea Stand United ya Shinyanga kwa mkataba wa miezi sita, ukiwa ni usajili wao kwanza dirisha hili.

Masota ameanza vizuri msimu huu baada ya kurejea kutoka kwenye majeraha ya goti yaliyomuweka nje ya uwanja kwa mwaka mmoja tangu alipoumia Desemba 21, 2023 akiwa na Geita Gold, ambapo alirejea uwanjani mwanzoni mwa msimu huu alipojiunga na Stand United.

Akiwa na Stand msimu huu katika Ligi ya Championship, Masota amecheza mechi 11, akifunga mabao mawili na asisti nne.

MASO 01

Akizungumzia kurejea kwake ndani ya Geita Gold aliyokuwa nayo msimu wa mwaka 2023/2024 Ligi Kuu Bara, Masota aliliambia Mwanaspoti ana deni kubwa kwa benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo ambao wamemuamini na kumpa nafasi.

“Nimefurahi kurejea nyumbani na nimefurahishwa na mapokezi makubwa ambayo timu na benchi la ufundi wamenipatia, naamini kwangu ni deni kubwa sana kwa mashabiki na wapenzi wa Geita Gold,” amesema Masota.

Amesema baada ya kutoka kwenye majeraha ya upasuaji wa goti, matarajio yake ilikuwa ni kupata timu yenye ushindani, hivyo kujiunga na Geita Gold ni hatua kubwa kwake, huku akiahidi makubwa kwa mashabiki wa timu hiyo.

MASO 02

“Nilikuwa natamani nipate timu yenye ushindani mkubwa kama Geita Gold na kuipambania kurejea tena Ligi Kuu kwa sababu naamini ni kiu ya wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wa Geita,” amesema Masota na kuongeza;

“Mashabiki watarajie mengi, lakini kubwa ni mimi kama mchezaji wao kupambania nembo ya Geita na kuifanya irudi Ligi Kuu kama matarajio yao.”