Miaka 62 ya Mapinduzi, nongwa, ubaguzi, shuruti ya uzalendo

Wito ulioijengea ushawishi agenda ya Mapinduzi Zanzibar, Januari 12, 1964, ulikuwa kuwaondoa Waarabu kwenye utawala, nyuma ya matamshi yaliyonadiwa ndani ya kampeni ya kumfukuza Sultan. Kwamba, Waarabu waachie madaraka, Wazanzibari asilia wajitawale.

Changamoto ambayo imebaki kuwa urithi (legacy) kuhusu Mapinduzi ni tafsiri. Wazanzibari wenye Upemba mwingi, tafsiri yao ya kiimani ni kuwa Unguja iliipindua Pemba. Wazanzibari wanaoifia zaidi Unguja, huamini Mapinduzi, siyo tu yalilenga kumwondoa Sultan, bali pia kuikomboa Pemba kwenye makucha ya Waarabu.

Wazanzibari ambao uhafidhina wao unafungamana zaidi na Upemba, hutafsiri kwamba Mapinduzi yalikuwa mkakati wa Tanganyika kuitwaa Zanzibar, na kilele chake ni Aprili 26, 1964, ilipoundwa dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kabla ya kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Changamoto hiyo ya kuwa na tafsiri tofauti ya Mapinduzi kutoka Unguja hadi Pemba, ndiyo zao la nongwa ya miaka 62, hisia za ubaguzi na kinachoonekana ni shuruti ya uzalendo na utii wa Mapinduzi tangu siku yalipofanyika. Mpaka leo, bado kuna makundi mawili ya Wazanzibari; wanaotamka ‘Mapinduzi Daima’ na wasiotamka. Halafu, kuna wanaotamka kinafiki.

Unguja, ndiyo hujinasibu kuwa wenye Mapinduzi na hutamka kwa sauti kubwa; ‘Mapinduzi Daima’. Pemba, wenaoitikia ‘daima’ kila linapotajwa neno ‘Mapinduzi’, huonekana wasaliti au wasio wazalendo kwa kisiwa chao. Wanamapinduzi daima, huwaona wasiotamka kuwa si Wazanzibari. Halafu, wale ambao ndimi zao ni muhali kusema ‘Mapinduzi Daima’, huwatafsiri Wanamapinduzi Daima kama walioiuza Zanzibar yao kwa Tanganyika.

Ufahari wa Mapinduzi kwa upande mmoja wa Wazanzibari na ukakasi uliopo kwa wengine, chanzo chake ni waasisi wa Mapinduzi. Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, hakufanya ipasavyo kuwafanya Wazanzibari wote waelewe dhana nzima, sababu na msukumo wa kufanya Mapinduzi.

Sheikh Karume, baada ya kufanikisha maandamano, alijielekeza zaidi katika kujenga vitu kwa usawa baina ya Pemba na Unguja, ili kudhihirisha kuwa visiwa hivyo ni pacha. Bahati mbaya, hakuwekeza kwenye utoaji elimu kwa umma, vilevile kujenga uenezi wa makundi au kutoka mtu mmoja hadi mwingine kuhusu Mapinduzi, umuhimu na ulazima wake.

Dhamira ya Karume ilikuwa njema, kuvifanya visiwa vyote viwili kupiga hatua za kimaendeleo kwa namna ya saresare. Hiyo ndiyo sababu ukifika Unguja utakutana na maghorofa marefu chini, ya Michenzani, kisha ukiwa Pemba, utayaona majengo ya Mapinduzi, Kengeja (Mkoani), Madungu, Machomane (Chakechake), Wete, Micheweni na Konde.

Karume alipokuwa anajenga usawa Zanzibar, alitaka kila chenye kufanyika Unguja, kifanyike pia Pemba, kwa ukubwa na ubora sawa. Kipindi akiwa madarakani, aliwapangia naibu mawaziri wote waishi Pemba, kusudi kila kilichokuwa kinaamuliwa na Baraza la Mapinduzi, kitekelezwe ipasavyo Pemba chini ya usimamizi wa naibu mawaziri.

Kama Karume alivyojenga kiwanja cha kuchezea watoto Kariakoo, Unguja, ndivyo alifanya hivyohivyo Tibirizi, Pemba. Mgawanyo wa ajira, Karume alitaka usawa, isipungue asilimia 60 kwa 40. Ikiwa ajira ni 100, basi Pemba waajiriwe kuanzia 40 kupanda juu.

Yalikuwa maono kuwa usawa wa huduma, miundombinu na vitu vingine vyenye kuonekana, ungeweza kuwafanya Wazanzibari kujiona ni kitu kimoja. Inasikitisha kuwa hilo halikufanikiwa. Bahati mbaya zaidi, imebaki kuwa hivyo kwa miaka yote 62. Hakuna upande wa kulaumiwa, haupo wenye kustahili pongezi.

Miaka 62 imetimia, bado kukiwa na kumbukumbu kuwa moja ya zawadi bora zaidi kuwahi kuwa nayo kama Watanzania, Dk Salim Ahmed Salim, hakupewa fursa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu ya historia ya Mapinduzi. Kumbukumbu mbaya za Salim na urais wa Tanzania ni Uchaguzi Mkuu 1985 na 2005.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipokuwa anakaribia kukabidhi kijiti cha uongozi wa nchi mwaka 1985, alikusudia kumkabidhi Salim. Simulizi hii inathibitishwa na Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Spika wa Nne, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa.

Mkapa alisimulia kupitia kitabu chake, “My Life, My Purpose”, Msekwa, alifafanua kwamba sababu ya Nyerere kushindwa kumkabidhi Salim kijiti ni msimamo wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Kwa mujibu wa Msekwa, wajumbe wa NEC walimgomea Nyerere kumsimamisha Salim kuwa mgombea urais, wakati alikuwa Waziri Mkuu, huku Mwinyi, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, ndiye alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania. Kiitifaki, Mwinyi alikuwa ngazi ya juu kuliko Salim.

Kwamba wajumbe wa NEC walisema haikuwa ikitoa tafsiri nzuri, kumteua Waziri Mkuu kuwa mgombea urais na kumwacha Makamu wa Rais. Ni kwa sababu hiyo, Msekwa alisema Mwalimu Nyerere alikwama katika mpango wake huo. Mwinyi akawa Rais, Salim akabanwa na Katiba kupata uteuzi wa Uwaziri Mkuu. Wakati huo, Katiba haikuwa ikiruhusu Rais na Waziri Mkuu kutoka sehemu moja ya Muungano. Mwinyi na Salim wote ni Wazanzibari.

Mwinyi, kupitia kitabu chake ‘Mzee Rukhsa; Safari ya Maisha Yangu’, amesimulia kwa undani kisa cha Salim kukataliwa. Mwinyi ameandika kuwa historia ya Mapinduzi ndiyo kikwazo kwa Salim. Hoja iliyopenyezwa ni kuwa Salim huwa hasemi ‘Mapinduzi Daima’. Zaidi, waliompinga wakadai Salim alihusika na mauaji ya Sheikh Karume, aliyeuawa kwa mapigo ya risasi, Aprili 7, 1972.

Tuweke pembeni mjadala wa kifo cha Karume, halafu tujadili suala la Mapinduzi. Kwa nini Salim alinyimwa fursa kwa sababu eti hatamki ‘Mapinduzi Daima’, wakati kipindi ambacho NEC inasimama imara kumgomea Mwalimu Nyerere na mpango wake, ilikuwa imeshakatika miaka 21 tangu Mapinduzi yatokee? Inajenga uthibitisho ni kiasi gani Mapinduzi yametengeneza nongwa ya kihistoria.

Salim ni kielelezo kuwa Mapinduzi yamejenga ubaguzi wa kihistoria Zanzibar. Asili yake ni Mpemba, na kwa vile propaganda ilijengwa kumzunguka kwamba hasemi ‘Mapinduzi Daima’, kwa hiyo Wazanzibari wenye kutamka ‘Mapinduzi Daima’, kwa sauti kubwa, wakaona Salim siyo Mzanzibari kamili, hivyo hana uzalendo.

Hata Uchaguzi Mkuu Tanzania mwaka 2005, Salim alishughulikiwa kwa sababu ya Mapinduzi. Aliitwa Hizbu, kwa maana ya Mwarabu, ambaye ndiye hasa upande wa waliopinduliwa. Salim ni kielelezo cha wengi ambao wamejeruhiwa kwa sababu ya ubaguzi uliozaliwa na Mapinduzi. Imeshindikana kufuta historia hiyo iliyojaa nongwa. Haijawezekana kuyafanya Mapinduzi kuwa fahari ya Wazanzibari wote. Hata wenye kusema ‘Mapinduzi Daima’, hutazamana baina ya wanaoita ‘Mapinduzi Matukufu’ na wasioyaita matukufu.

Rwanda, Rais Paul Kagame, baada ya kuishika dola kwa mikono yote miwili, aliharamisha baadhi ya maneno kutakwa ili kuzifanya jamii mbili za Kinyarwanda, Wahutu na Watutsi, wapendane bila kuuona au kuuhisi ubaguzi baina yao. Hata hivyo, huo umebaki kuwa uzalendo wa shuruti.

Wanyarwanda wanaogopa kutamka maneno yaliyoharamishwa kisheria Rwanda, lakini nyoyo zao bado zina ubaguzi. Wahutu wanaamini kwamba mbaguzi namba moja Rwanda ni Kagame. Huo ndiyo msimamo wa vikundi vya waasi Rwanda. Hayo ndiyo maneno yanayoishi ndani ya vifua vya Wanyarwanda jamii ya Wahutu.

Huo ni mfano ambao unafanana kwa ukaribu na Zanzibar. Kuna shuruti ya kutamka ‘Mapinduzi Daima’ ili uonekane mzalendo. Naomba kufafanua; wakati Rwanda kuna maneno yamepigwa marufuku kutamkwa ili Wanyarwanda kwa kutoyatamka ndiyo waonekane wazalendo, Zanzibar, unalazimishwa kusema ‘Mapinduzi Daima’, utambuliwe kuwa mzalendo. Ni kupitia mfano wa Salim, kama alivyosimulia Mwinyi.

Uzalendo haupaswi kuwa wa shuruti, bali utashi binafsi na kwa mahaba ya dhati. Wazanzibari wanatakiwa kuyapenda na kuyaenzi Mapinduzi kwa moyo wote, siyo kwa kushurutishwa au kutamka Mapinduzi Daima’ kwa unafiki ili kutojizibia fursa. Itawezekana kama elimu itatolewa kikamilifu, kizazi kimoja baada ya kingine. Muhimu, kufanya uwekezaji mkubwa katika kufuta mbegu ya ubaguzi ambayo huambukiza kizazi kimoja hadi kingine.

Hata sura ya kisiasa Zanzibar, Pemba kuonekana kuwa ngome ya upinzani, wakati Unguja, CCM ikitamalaki, sababu ni historia ya Mapinduzi. Mbegu ya ubaguzi haikufutwa. Nongwa ikaachwa ishamiri. Halafu uwekezaji wa kushurutisha matamshi ya ‘Mapinduzi Daima’, ukaongeza mgawanyiko. Sheikh Karume alijitahidi kwa kuwekeza vitu, maono yake hayakusaidia. Marais sita waliofuata baada yake, hawajafanikiwa kuyafanya Mapinduzi kuwa fahari ya Wazanzibari wote. Pengine wa sasa, Dk Hussein Mwinyi, au mwingine baada yake.