Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema katika miaka 62 ya mapinduzi, wanajivunia jitihada zilizofanyika na kupata mafanikio ya kukuza uchumi na sekta zingine kama ilivyokuwa malengo ya mapinduzi hayo.
Dk Mwinyi amesema hayo leo Jumatatu kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) ikiwa ni kilele cha kuadhimisha miaka 62 ya mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964.
Dk Mwinyi amesema Serikali ya awamu ya nane ilipoingia madarakani iliahidi kudumisha mafanikio ya awamu zote zilizotangulia ya uongozi na kuyatafsiri mapinduzi kwa vitendo na kuleta mageuzi ya kiuchumi na kisiasa kwa manufaa ya wananchi wote, jambo ambalo wamefanikiwa.
Amesema uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika vyema, mwaka 2024 ulikuwa kwa kasi ya asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 1.3 mwaka 2020, huku bei ya soko ikiongezeka kufikia Sh6.5 trilioni kwa mwaka 2024 kutoka Sh4.78 mwaka 2021.
“Ukusanyaji wa mapato umetoka Sh856 bilioni hadi kufikia Sh2.1 trilioni, tukifanikiwa kudhibiti kasi ya mfumko wa bei kubaki katika tarakimu moja na kubaki asilimia tano,” amesema.
Dk Mwinyi amesema kasi ya uwekezaji, hadi kufikia Desemba 2025 miradi 1,657 yenye mtaji wa Dola 20.2 bilioni za Marekani ilisajiliwa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) ikihusisha utalii, viwanda na nyumba za biashara ambayo inatarajiwa kutoa ajira 87,696.
Amesema Serikali imeimarisha maeneo ya kimkakati ya uwekezaji ya Micheweni na Fumba; na itaendelea kuweka vivutio vya wawekezaji katika sekta za uchumi wa buluu, viwanda, nishati mbadala, anga, baharini na kilimo.
Kwa upande wa sekta ya utalii, amesema imeendelea kupewa kipaumbele kutokana na mchango wake kuongezeka na kufikia watalii 816,438 ambao wameingia Zanzibar mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 27 walioingia mwaka 2024.
Katika kuongeza watalii, wanadhamira ya kuongeza idadi ya matamasha, kuimarisha urithi wa majengo ya kale, michezo utamaduni, makongamano ya kitaifa na vivutio vya maumbile na asili.
Amesema sekta ya uvuvi imeimarika kwa asilimia 110 kutoka tani 38,107 mwaka 2020 hadi kufikia tani 78,943 mwaka 2024 huku mapato yakiongezeka kutoka Sh203 bilioni hadi kufikia Sh608 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 201.
Pia, uzalishaji wa mwani umeongezeka kutoka tani 8,785 zenye thamani ya Sh5.3 bilioni hadi kufikia tani 19,716 sawa na Sh16.4 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 94, huku sekta hiyo ikitoa ajira 100,000.
Akizungumzia sekta ya mafuta na gesi amesema wataendelea kuishugulikia kutoka hatua ya sasa ya ugawaji vitalu na kuvitangaza vitalu 10 kimataifa.
Kwa upande wa bandari, amesema zimeimarika, Bandari ya Mangapwani yenye uwezo wa kuhudumia makotena 200,000 na mizigo tani milioni moja imeanza kujengwa na inatarajiwa kukamilika mwaka 2028.
Akizungumzia huduma za usafiri, Rais Mwinyi amesema zimeendelea kuimarishwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Amesema safari za ndani zimeongeza kutoka 5,696 mwaka 2024 hadi 8,192 mwaka 2025 huku safari za kigeni kutoka 98 hadi 205.
Rais Mwinyi amesema meli za ndani 87 zimesajiliwa na meli 613 za kimataifa zimesajiliwa huku mapato yakiongezeka kufikia Sh8.2 bilioni ikilinganisha na Sh6.4 bilioni ya mwaka 2024.
“Mafanikio makubwa yamepatikana katika jitihada za Serikali kujenga barabara kuu za ndani na mijini, Serikali imekamilisha ujenzi wa kilometa 82.8 barabara za mjini na kilometa 247 za vijijini na daraja la juu la Mwankwerekwe.
“Daraja la Amani limefikia asilimia 30, Uzi Ng’ambwa asilimia 70 na Pangatupu limefikia asilimi 90,” amesema Dk Mwinyi.
Akieleza mafanikio katika sekta ya anga, amesema idadi ya abiria imeongezeka kutoka 2,133,166 mwaka 2023/24 hadi kufikia 2,578,250 mwaka 2024/25 na idadi ya mizigo iliyohudumiwa kutoka tani 4,224 hadi tani 4,603 huku ujenzi wa jengo jipya la abiria ukiendelea na uwanja wa ndege wa Pemba tayari umeanza kujengwa.
“Kwa upande wa ardhi na makazi, tunapoadhimisha miaka 62 ya mapinduzi, Serikali imeimarisha sekta ya ardhi kwa kuandaa hati za matumizi ya radhi 1,577 na kuimarisha upatikanaji wa ukodishwaji ardhi 399 ili kuendeleza shughuli za uwekezaji,” amesema Rais Mwinyi.
Amesema jumla ya viwanja 961 vimepimwa kwa ajili ya maeneo ya makazi, taasisi, mashamba na vitega uchumi.
Rais Mwinyi amesema Serikali imeimarisha sekta ya kilimo inayoajiri asilimia 35 ya wananchi, hivyo kuna tija katika kilimo cha mpunga baada ya kukamilisha mabonde ya umwagiliaji yenye ukubwa wa hekta 1,325 na kuyagawa kwa wakulima.
“Serikali ina lengo kuongeza uzalishaji wa mpunga kufikia tani 15 kwa ekari kwa mwaka na kuimarisha huduma ya ugani kuwapatia wakulima vifaa vya kisasa na kujenga maghala ya kuhifadhia chakula,” amesema.
Katika kuwaendeleza wajasiriamali, mikopo 6,238 yenye thamani ya Sh50.7 bilioni imetolewa kwa wananchi 27,563 kwa sekta mbalimbali.
Pia, Serikali imejenga masoko manne katika Mkoa wa Mjini Magharibi na masoko mengine madogo 11.
Katika kukabiliana na changamoto za ajira hususani kwa vijana, Serikali inaendelea kuvisaidia vikundi 1,263 vilivyoanzishwa na klabu za wanachama 3,796 huku miradi 37 ya vijana yenye thamani ya Sh28 bilioni ikitekelezwa kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo.
Uimarishaji wa huduma za jamii ikiwamo elimu, afya, majisafi na salama ni miongoni mwa malengo ya mapinduzi, hivyo Serikali imeifanya sekta ya elimu kuwa kipaumbele na mageuzi makubwa yamefanywa.
Rais Mwinyi amesema kumekuwa na ujenzi wa shule za kisasa za ghorofa 35, kupatikana vifaa vya kisasa na mazingira ya kufundishia ambavyo vimechangia kuimarisha mazingira mazuri ya kuongeza ufaulu.
Ili kwenda sambamba na mageuzi ya elimu ya mtalaa mpya, amesema jumla ya shule 70 zitaunganishwa na mkonga wa mawasiliano, kompyuta 2000 na laptop 4000 vitatolewa na kufundisha kupitia Tehama.
“Serikali imepanga kuajiri walimu wapya 500 kupunguza uhaba wa walimu hasa wa sayansi na kuendelea kujenga ujenzi wa mabweni na kuimarisha masilahi na kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu,” amesema Rais Mwinyi.
Kuhusu afya, amesema wameimarisha mfumo wa rufaa na kukamilika kwa hospitali za wilaya na kuongeza idadi ya watumishi wa afya.
“Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za majisafi na salama, tumefanikiwa kuongeza visima vya maji kufikia 455 kutoka 308 vyenye uwezo wa kuzalisha lita 5.9 milioni kwa sasa sawa na lita za maji milioni 143 kwa siku,” amesema Rais Mwinyi.
Pia, amesema wamejenga matangi ya kuhifadhi maji 87, matangi 25 yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 144 yamejengwa kupitia mradi wa mfumo wa usambazaji maji wa Exim Bank ya India na mradi usambazaji maji kwa fedha za Uviko-19.
Katika sekta hiyo, amesema wameongeza mtandao wa maji kufikia kilometa 2,080 za mabomba, jumla ya wateja wapya 31,357 wamesajiliwa na kuunganishwa na mtandao wa maji na baada ya kukamilika mradi wa Exim, jumla ya nyumba 5,820 zimeunganishwa na huduma za maji.
Kwa mwaka huu, amesema Serikali itatekeleza mradi mkubwa wa maji Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkoa wa Kusini Unguja.
Hata hivyo, amesema kupitia Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca) kati ya Januari hadi Desemba 2025 wameokoa Sh6.6 bilioni na Dola 94,370 za Marekani, kesi za wahusika zipo katika hatua mbalimbali huku hati safi za ukaguzi zikiendelea kuongezeka.
