ALIYEKUWA mshambuliaji wa Simba Queens, Magnifique Umutesiwase amerejea nchini kwao Rwanda kujiunga na Indahangarwa inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake huko.
Hatua hiyo ya Magnifique inakuja miezi michache baada ya Simba Queens kuamua kuachana naye mwishoni mwa mwaka jana ikidaiwa alishindwa kuendana na kasi pamoja na mahitaji ya kikosi hicho, hususan katika eneo la ushambuliaji.
Magnifique alitarajiwa kuingiza ushindani eneo la ushambuliaji wanalocheza Jentrix Shikangwa, Aisha Mnunka, Zawadi Usananse, Cynthia Musungu na Zainah Nandede.
Lakini tangu asajiliwe mshambuliaji huyo alikosa namba mbele ya wachezaji hao na kujikuta akiishia kukaa benchi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Simba, benchi la ufundi liliona mchezaji huyo ameshindwa kubeba majukumu makubwa ya ushambuliaji, hali iliyosababisha klabu hiyo kuchukua uamuzi wa kusitisha mkataba naye.
“Eneo la ushambuliaji lina wachezaji wengi na wanaonyesha ushindani mkubwa tukaona ni bora tusitishe mkataba naye ili tupate nafasi ya kuongeza wachezaji wengine hasa eneo la ulinzi bado lina changamoto,” kilisema chanzo.
Hata hivyo, kurejea kwake nyumbani kunaonekana kumpa nafasi mpya ya kufufua matumaini kwake, kwani tayari ameanza kupata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi hicho.
Baada ya kuachana na Wanamsimbazi Magnifique alikuwa miongoni mwa wachezaji waliopata dakika za kucheza katika fainali ya Super Cup, Rayon ikinyakua taji hilo baada ya kuitandika chama la nyota huyo mabao 4-0.
