Simba yabeba kombe Mwanza, yaichapa Pamba 3-2

Mashabiki wa Simba wameifutia aibu timu yao na kuipatia kombe baada ya muda mrefu kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo wa kirafiki kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

‎Mchezo huo ambao umeandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, umechezwa leo Jumatatu Januari 12, 2025 kuanzia saa 10 jioni katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Mashabiki na wachezaji wa zamani wa Simba na Pamba Jiji wamechuana katika mchezo huo uliovuta mashabiki wengi.

‎Mchezo huo, umesindikizwa pia na michezo mingine ikiwemo kuvuta kamba, kukimbiza kuku, mbio za mita 100 na kukimbia kwenye magunia.

‎Baada ya ushindi wa mabao 3-2, Simba imebeba kombe na zawadi ya Sh1 milioni, huku kipa wake, Wilbert Mweta akiibuka mchezaji bora wa mchezo, na Muslim Nassoro mfungaji bora kwa kutupia kambani mabao mawili.

 Pamba imeambulia zawadi ya mshindi wa pili ya Sh300,000.

‎Akizungumzia mchezo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewapongeza viongozi na mashabiki wa Simba kwa mwitikio mkubwa na kujitokeza kwa wingi.

‎Kutokana na kilichofanywa na Wekundu wa Msimbazi, Mtanda ameahidi kuendelea kuwa mlezi mzuri wa Simba mkoa wa Mwanza na kuwaunga mkono katika shughuli zao wakati wowote.

‎”Nawapongeza viongozi wa Simba kwa kujipanga vizuri, nawapongeza pia mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi. Mtani (Yanga) ameogopa kushiriki labda maandalizi yake yalikuwa dhaifu,” amesema Mtanda na kuongeza:

‎”Viongozi wa Simba mkoa wa Mwanza wamejipanga vizuri, wana uongozi imara. Mimi nitaendelea kuwa mlezi wa Simba Mwanza.”