Stanbic yatajwa tena benki bora Tanzania mwaka 2025

Dar es Salaam. Kwa mara nyingine tena Stanbic imetajwa kuwa Benki Bora zaidi Tanzania kwa mwaka 2025 na jarida la The Banker, chapisho la kimataifa la masuala ya benki chini ya Financial Times.

Tuzo hii inatambua utendaji mzuri wa kifedha wa benki, ubunifu na mchango wake endelevu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na hii ni mara ya nane kwa Stanbic kupokea heshima hii, jambo linaloimarisha nafasi yake kama moja ya taasisi za kifedha zinazoaminika na kudumisha viwango vya juu Tanzania.

Katika soko lenye ushindani mkubwa kama Tanzania, tuzo hii inatambua mchango mkubwa wa Stanbic katika sekta muhimu za uchumi wa Tanzania ikiwamo nishati na miundombinu, pamoja na kuendeleza ubunifu unaosaidia ukuaji wa biashara ndogo na za kati.

Katika kipindi cha hadi kufikia Juni 2025, Stanbic iliunga mkono ajenda ya viwanda ya Tanzania kwa kutoa zaidi ya Dola 1 bilioni Marekani (Sh2.5 trilioni), katika uwezeshaji wa maendeleo kwenye sekta za nishati, usafirishaji na zingine.

Uwezeshaji huu uliwezesha utekelezaji wa miradi muhimu ya miundombinu ya kitaifa ikiwamo uboreshaji wa bandari, upanuzi wa gridi ya Taifa ya umeme na uwezeshaji katika mnyororo wa thamani wa gesi asilia.

Jarida hilo la Uingereza pia lilitambua mchango wa Stanbic katika kuleta athari chanya kwa Watanzania.

Kupitia uwekezaji wa kijamii katika elimu, afya, mazingira na elimu ya kifedha.

Benki iliwanufaisha zaidi ya watu milioni 2 walioko sehemu mbalimbali nchini kwa mwaka 2025.

Kiatamizi cha Stanbic Biashara Incubator kiliwafikia wajasiriamali takribani 5,000 kwa kuwapatia stadi za ujuzi wa vitendo uliowawezesha kuongeza uelewa wa kifedha, biashara, matumizi ya nishati safi na ushiriki katika fursa za biashara.

Akizungumza kuhusu tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira, amesema tuzo hiyo inaakisi historia ya benki na dira yake ya baadaye.

“Tunajivunia kutajwa kuwa Benki Bora Tanzania kwa mwaka 2025. Tuzo hii inatambua safari yetu ya miaka 30 nchini Tanzania na inathibitisha dhamira yetu kwamba Tanzania ni nyumbani kwetu na tunachangia ukuaji wake,” amesema Rwegasira.

Amesema katika Katika mwaka uliopita, waliwekeza mitaji katika miradi ya kimkakati katika sekta za nishati, biashara na miundombinu sanjari na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia suluhisho za kidijitali na kuchochea uwekezaji katika biashara za kikanda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko wa Stanbic Bank Tanzania, Neemarose Singo amesema tuzo hiyo ni matokeo ya juhudi za wafanyakazi wa benki na imani kubwa waliyonayo wateja wao.

“Tuzo ya Benki Bora ni uthibitisho wa kazi kubwa iliyofanywa na timu zetu kote nchini. Inatambua nidhamu yetu, ubunifu wetu na dhamira yetu ya kuwezesha biashara, familia na jamii kukua. Tunajivunia hatua hii na tunawashukuru wateja wetu kwa kuendelea kuchagua Stanbic kama mshirika wao,” amesema.

Ameongeza kuwa mwaka 2025 ulikuwa wa kihistoria kwa benki, ulioshuhudia ufunguzi wa matawi mapya, matumizi mapana ya huduma za kidijitali, shughuli imara za masoko ya mitaji na kuendelea kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.