MSHAMBULIAJI nyota wa Singida Black Stars, Mzambia Andrew Phiri, ameenda Ureno katika majaribio katika timu ya Clube Desportivo Nacional, baada ya uongozi wa kikosi hicho kumridhia kwa lengo la kwenda kujaribu bahati yake barani Ulaya.
Phiri aliyejiunga na kikosi hicho Agosti 26, 2025, akitokea Maestro United ya kwao Zambia, mkataba wake unafikia tamati rasmi Juni 30, 2028, ingawa baada ya dili hilo kutokea pande hizo zote mbili zimemruhusu nyota huyo kwenda huko Ureno.
Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti Phiri ameenda Ureno kujaribu bahati yake na endapo atafaulu wako tayari kumuachia moja kwa moja, hivyo, makubaliano yaliyofikiwa ni ya pande mbili kati ya kambi ya mchezaji na uongozi.
“Sisi hatuna lengo la kumzuia mchezaji yoyote tunayeona ana nafasi ya kuzidi kuonekana zaidi ya hapa kwetu alipo, baada ya uongozi wa Nacional kumuhitaji Phiri akafanye majaribio tukaona ni vizuri tumuachie aende,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, chanzo hicho kilisema nyota huyo ana nafasi ya kurudi ikiwa majaribio yake yataenda vibaya kwa sababu bado ana mkataba, ingawa lengo lao kama uongozi ni kuona anafanikiwa ili kutoa hamasa wa wengine kuzidi kupambania ndoto zao.
Phiri aliyezaliwa Mei 21, 2001, alifanya pia majaribio Orlando Pirates ya Afrika ya Kusini Machi 2025, ambako alimaliza mfungaji bora wa Maestro United kwa misimu minne mfululizo, huku akiifungia timu hiyo mabao 69, kwenye mashindano yote.
Mwanzoni mwa msimu, nyota huyo alikuwa anahusishwa na timu za Zesco United na Power Dynamos zote za kwao Zambia, baada ya kuonyesha kiwango kizuri kilichoivutia miamba hiyo, huku kwa msimu wa 2023-2024, akichaguliwa mchezaji bora wa msimu.
Pia, mshambuliaji huyo kabla ya kujiunga na Singida msimu huu, alikuwa akihusishwa na miamba wa soka hapa nchini Yanga, Simba, Azam, huku Pamba Jiji ikijitosa kumuwania na kushindwa kiasi cha fedha kilichohitajika kutoka kwa Maestro United.
Katika Ligi Kuu ya Ureno, kabla ya mechi ya jana dhidi ya Santa Clara, Nacional iko nafasi ya 14 kwaa pointi 16, baada ya kushinda mechi nne, sare nne na kupoteza nane kati ya 16 ilizocheza msimu huu, huku ikifunga mabao 18 na kuruhusu 23.
