Tanroads Kigoma yatangaza donge kwa watakaofanikisha kukamatwa kwa wezi

Kigoma. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Kigoma, imetangaza zawadi kwa mwananchi atakayefanikisha kukamatwa kwa wezi wanaoiba vyuma vinavyoonesha alama za barabarani mkoani humo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Januari 10, 2026 na ofisi ya Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kigoma Mhandiai Narcis Choma yeyote atakayefanikisha au kutoa ushahidi huo atapewa zawadi mpaka Sh150,000  kulingana na ushahidi.

Taarifa  hiyo inaeleza kuwa,  “Meneja wa Wakala ya Barabara Mkoa wa Kigoma anasikitika kuwajulisha wananchi wote kuwa kumekuwepo na ongezeko la matukio ya wizi wa alama za barabarani, taa za barabarani, uvunaji wa mchanga kwenye mitaro pamoja na vyuma vya madaraja katika maeneo mbalimbali ya mkoa wetu.”

Taarifa hiyo inaongeza kuwa, “vitendo hivi vinasababisha hasara kubwa kwa Serikali, kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara, madaraja pamoja na kuathiri maendeleo ya miundombinu, Serikali kwa kushirikiana na Tanroads, inawaomba wananchi wote kutoa taarifa na kufichua wahusika wanaofanya vitendo vya wizi huo.

Baadhi ya alama za barabarani mkoani Kigoma, zikiwa zimekatwa na watu wasiojulikana ikitajwa kushamiri kutokana na biashara ya vyuma chakavu.

Aidha, zawadi nono ya fedha taslimu kuanzia Sh150,000 na zaidi itatolewa kulingana na uzito wa tukio litakaloibuliwa huku mtoa taarifa akilipwa kupitia simu yake ya mkononi kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zenye ushahidi na zitakazowezesha kuwatia mbaroni wahalifu wanaoiba au kununua alama za barabarani, taa za barabarani na vyuma vya madaraja au hata taarifa itayopelekea kuiokoa miundombinu hiyo kuibiwa.

Wizi wa alama za barabarani katika Manispaa ya Kigoma, imehusishwa na biashara ya vyuma chakavu ambapo mpaka sasa zaidi ya alama 50 za barabarani, zimeibwa huku taa za barabarani pia zikidaiwa kuibwa.

Leo Jumatatu Januari 12,2026,Mwananchi imemtafuta kwa njia ya simu, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kigoma Narcis Choma ambaye amethibitisha taarifa hiyo huku akibainisha kuwa fedha hizo za zawadi zimetolewa na wadau wenye uchungu na miundombinu hiyo.

“Tumetoa namba yetu ya WhatsApp ambayo mtu atatuma video au picha, tukijiridhisha tutamtumia pesa yake hatuhitaji hata kukuona na tunakulinda, hii miundombinu ni ya kwao inatakiwa wailinde” Amesema Mhandisi Choma.

Kutokana na kuibwa kwa miundombinu hiyo la alama za barabarani, Choma amesema kunaathiri hali ya usalama kwa watumiaji wa barabara, kwa kuwa ili kurejesha upya alama hizo hadi pale itakapojumuishwa katika bajeti ijayo kwakuwa inategemeana na bajeti ya mwaka husika.

Baadhi ya alama za barabarani mkoani Kigoma, zikiwa zimekatwa na watu wasiojulikana ikitajwa kushamiri kutokana na biashara ya vyuma chakavu.

Choma amewataka wananchi wanaofanya shughuli za ukusanyaji mchanga katika mitaro ya barabara, kuacha mara moja kwa kuwa imesababisha mitaro mingi na kingo za Barabara kubomoka hasa kipindi hiki cha Mvua nyingi.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dk Rashid Chuachua akizungumza kwa njia ya simu, ametoa wito kwa wananchi kuilinda miundombinu yote ya maendeleo kwa kuwa ina tija kwa maendeleo ya mkoa.

“Kwa muda mrefu Kigoma haikuwa na miundombinu bora ya barabara sasa imepatikana baadhi wasio wema wanaharibu, nitoe wito kwa wananchi sio tu katika miundombinu ya barabara, hata miradi mingine ya maendeleo tushirikiane kuilinda kwa faida yetu.”