MBEYA City inaendelea na maboresho dirisha hili dogo la usajili na kikosi hicho kutoka jijini Mbeya kiko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa aliyekuwa beki wa kulia wa Singida Black Stars, Kelvin Kijili.
Beki huyo aliyejiunga na Singida Julai 11, 2025, akitokea Simba, awali alikuwa katika mazungumzo ya kujiunga na kikosi cha TRA United zamani Tabora United, japo Mbeya City imeingilia kati dili hilo na muda wowote kuanzia sasa itamtangaza.
Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa Mbeya City, kimeliambia Mwanaspoti Kijili tayari amemalizana na mabosi wa timu hiyo ya Mbeya na muda wowote kuanzia leo Jumanne atajiunga na nyota wenzake kwa ajili ya kuanza mazoezi na kikosi hicho.
“Taratibu zote za kumpata zimekamilika na kilichobakia na mambo madogo tu ambayo kuanzia leo Jumanne pande zote mbili kwa maana ya mchezaji na uongozi itazikamilisha ili aungane na wachezaji wenzake kikosini kwetu,” kilisema chanzo hicho.
Kijili ameachana na Singida baada ya ujio wa Abdallah Said Ali ‘Lanso’ aliyesajiliwa akitokea KMC akiungana na kiungo, Said Naushad aliyeachana na MFK Karvina B ya Jamhuri ya Czech aliyojiunga nayo akitokea timu ya Kagera Sugar.
Nyota wengine wapya katika kikosi hicho kinachonolewa na Kocha, Mecky Maxime ni Abalkassim Suleiman aliyeachana na Pamba Jiji tangu msimu uliopita na aliyekuwa kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana aliyevunja mkataba wake na timu hiyo.
Mwingine ni aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Yacouba Songne raia wa Burkina Faso, ambaye anakaribia kujiunga na kikosi hicho pia, baada ya msimu wa 2024-2025 kuachana na TRA United zamani Tabora United aliyoifungia mabao manne ya Ligi Kuu.
