Dubai. Rais wa Marekani, Donald Trump amesema nchi yake inaweza kukutana na maofisa wa Iran na kwamba tayari iko katika mawasiliano na makundi ya upinzani, huku akitafakari wigo mpana wa majibu makali ikiwamo kutumia nguvu za kijeshi kufuatia ukandamizaji wa kikatili wa maandamano nchini Iran.
Kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera, maandamano hayo yanatajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zaidi kwa utawala wa kidini tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Wakati maandamano hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi amesema maandamano hayo yamekuwa na vurugu kwa sababu baadhi ya wahalifu wanataka kumridhisha Trump ili Marekani iingilie kati mzozo huo.
“Tuko tayari kwa vita, lakini pia tuko tayari kwa mazungumzo,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Araqchi, leo, alipokuwa akitoa taarifa kwa mabalozi wa nchi za nje jijini Tehran kupitia tafsiri ya Kiingereza.
Katika hatua nyingine, Trump amewatahadharisha viongozi wa Iran kwamba Marekani itachukua hatua za kijeshi endapo vikosi vya usalama vitatumia risasi dhidi ya waandamanaji.
Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake Marekani, HRANA, limesema limethibitisha vifo vya waandamanaji 490 na askari 48 wa vyombo vya ulinzi, huku zaidi ya watu 10,600 wakikamatwa.
Serikali ya Iran haijatoa takwimu rasmi za vifo, na mashirika ya habari hayajaweza kuthibitisha kwa njia huru idadi hiyo.
Trump alisema jana kuwa Iran imewasiliana na Marekani ikitaka mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia, ambao uliwahi kushambuliwa na Israel na Marekani katika vita vya siku 12 vilivyotokea Juni 2026.
“Ndiyo, Iran inataka majadiliano. Huenda tukakutana nao. Mpango wa mkutano unaandaliwa, lakini huenda tukalazimika kuchukua hatua kutokana na yanayotokea kabla ya mkutano huo. Hata hivyo, maandalizi ya mkutano yanaendelea. Iran ilipiga simu, wanataka mazungumzo,” Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya rais, Air Force One.
Trump anatarajiwa kukutana na washauri wake wakuu kesho Jumanne kujadili mambo mbalimbali kuhusu Iran, ofisa mmoja wa Marekani aliiambia Reuters jana Jumapili.
Gazeti la The Wall Street Journal liliripoti kuwa miongoni mwa mambo hayo ni uchaguzi wa mashambulizi ya kijeshi, matumizi ya silaha za mtandaoni kwa siri, kupanua vikwazo vya kiuchumi, pamoja na kutoa msaada wa kidijitali kwa makundi yanayopinga serikali.
“Jeshi linafanyia kazi tathmini yake, nasi tunaangalia chaguo kali sana,” Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa kwenye Air Force One.
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, aliionya Marekani dhidi ya “makosa ya kimahesabu.”
“Tuwe wazi, endapo Iran itashambuliwa, maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel), pamoja na kambi na manowari zote za Marekani, zitakuwa malengo yetu halali,” amesema Qalibaf, aliyewahi kuwa Kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Makaburi na mifuko ya maiti
Maandamano yalianza Desemba 28, 2025, yakichochewa na kupanda kwa kasi kwa gharama za maisha, kabla hayajageuka kuwa upinzani wa wazi dhidi ya watawala wa kidini walioko madarakani tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Wananchi wa Iran, wanaohangaika kujikimu kimaisha, wamezidi kuonesha hasira dhidi ya walinzi wa mapinduzi wenye nguvu kubwa, ambao masilahi yao ya kibiashara ikiwamo sekta ya mafuta na gesi, ujenzi na mawasiliano, yanakadiriwa kuwa na thamani ya mabilioni ya dola.
Televisheni ya taifa leo imerusha moja kwa moja picha za umati mkubwa wa watu waliohudhuria mazishi ya askari wa vyombo vya usalama waliouawa mjini Shahrud, pamoja na maandamano ya kuiunga mkono serikali katika miji kama Kerman, Zahedan na Birjand, yaliyofanyika “kulaani matukio ya hivi karibuni ya kigaidi.”
Vilevile, ilitangaza wito kutoka kwa maofisa wakuu mbalimbali ukiwahimiza wananchi kujitokeza mitaani Jumatatu.
Mamlaka za Iran zimeituhumu Marekani na Israel kwa kuchochea vurugu, na zimetangaza wito wa maandamano ya kitaifa leo kulaani, “vitendo vya kigaidi vinavyoongozwa na Marekani na Israel,” kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Araqchi amesema hali nchini Iran iko “chini ya udhibiti kamili” baada ya machafuko yanayohusiana na maandamano kuongezeka mwishoni mwa wiki. Ameongeza kuwa onyo la Trump kwa Tehran kuhusu kuchukua hatua endapo maandamano yangemwaga damu lilikuwa limewapa motisha “magaidi” kuwalenga waandamanaji na vikosi vya usalama ili kuchochea uingiliaji wa kigeni.
Mtiririko wa taarifa kutoka Iran umekumbwa na vikwazo kutokana na kuzimwa kwa intaneti tangu Alhamisi iliyopita. Jana, Trump alisema atazungumza na Elon Musk kuhusu kurejesha huduma ya intaneti nchini Iran kupitia mtandao wa satelaiti wa Starlink.
Araqchi amesema huduma ya intaneti itarejeshwa kwa uratibu na vyombo vya ulinzi.
Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii Jumamosi kutoka Tehran zilionyesha umati wa watu wakitembea usiku, wakipiga makofi na kuimba nyimbo za maandamano. “Umati huu hauna mwanzo wala mwisho,” sauti ya mwanaume mmoja ilisikia ikisema.
Televisheni ya taifa ilionesha mifuko kadhaa yenye maiti ikiwa imelazwa katika ofisi ya uchunguzi wa maiti jijini Tehran, ikisema waliokufa ni waathirika wa matukio yaliyosababishwa na “magaidi wenye silaha.” Ilionesha pia picha za ndugu na jamaa wakikusanyika nje ya Kituo cha Uchunguzi wa Kitabibu cha Kahrizak, Tehran, wakisubiri kutambua miili ya wapendwa wao.
Mamlaka zilitangaza jana siku tatu za maombolezo ya kitaifa “kwa heshima ya mashahidi waliouawa katika mapambano dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni,” kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Vyanzo vitatu vya Israel, vilivyohudhuria mashauriano ya kiusalama mwishoni mwa wiki, vilisema Israel ilikuwa katika tahadhari ya juu kutokana na uwezekano wa uingiliaji wowote wa Marekani.
Juni mwaka jana, Israel na Iran zilipigana vita vya siku 12, ambavyo Marekani ilijiunga kwa muda mfupi kwa kushambulia vituo vya nyuklia. Iran ilijibu kwa kurusha makombora kuelekea Israel na katika kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Qatar.
Ingawa mamlaka za Iran zimewahi kustahimili maandamano ya awali, machafuko ya sasa yanajitokeza wakati Tehran bado inajijenga upya baada ya vita vya mwaka jana, huku nafasi yake ya kikanda ikidhoofishwa na pigo kwa washirika wake, ikiwamo Hezbollah wa Lebanon, tangu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel.
Machafuko nchini Iran yanajiri wakati Trump akionesha msimamo mkali wa nguvu za Marekani kimataifa, baada ya kumuondoa madarakani Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na wakati huohuo kujadili mpango wa kununua kisiwa cha Greenland au kukitwaa kwa mabavu.
Alan Eyre, aliyewahi kuwa mwanadiplomasia wa Marekani na mtaalamu wa masuala ya Iran, amesema anaona ni vigumu maandamano hayo kuuangusha kabisa mfumo wa utawala.
“Naona kuna uwezekano mkubwa serikali kuyadhibiti maandamano haya, lakini itatoka katika mchakato huo ikiwa dhaifu zaidi,” ameiambia Reuters, akibainisha kuwa tabaka la juu la uongozi wa Iran bado linaonekana kuwa imara na hakuna upinzani uliopangwa kwa nguvu.
Trump, kupitia chapisho lake la mitandao ya kijamii Jumamosi, alisema: “Iran inaangalia uhuru, labda kwa namna isiyowahi kutokea kabla. Marekani iko tayari kusaidia!”
