Dodoma. Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), umekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari zikieleza uwepo wa changamoto ya uhaba wa mabweni kwa wanafunzi chuoni hapo.
Hayo yanajiri kufuatia malalamiko yaliotolewa na baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wiki iliyopita kupitia mitandao ya kijamii wakidai kuwa wanazimika kulala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja kutokana na ukosefu wa vyumba, huku wengine wakilazimika kupangisha licha kulipa hela ya malazi.
Wanafunzi hao walienda mbali zaidi na kudai kuwa mfumo wa usajili chuoni hapo (Sr2) unawalazimisha kulipia malazi (Accomodation Fees) ili kujisajili kwa muhula wa masomo ila wanapomaliza wanapewa taarifa kuwa vyumba vimejaa, hali inayowalazimu kubebana kulala wawili kwenye kitanda kimoja.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu malalamiko hayo, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Masoko chuoni hapo, Rose Mdami amesema taarifa hizo si za kweli kwani mpaka kufikia sasa vipo baadhi ya vyumba ndani ya chuo hicho ambavyo havina watu.
“Si kweli ila kilichopo ni kuwa wapo baadhi ya wanafunzi wanaolipa ada kidogokidogo kulazimika kuhifadhiwa kwa wenzao kwa sababu huwezi kupata chumba kama hujakamilisha usajili,” amesema Mdami.
“Lakini pia wapo ambao tunawapangia vyumba, ila hawataki kwenda walipopangiwa kwa sababu zao ikiwemo kutaka kukaa pamoja na marafiki zao au kuwa karibu na sehemu fulani hivyo hujikuta wakijikusanya sehemu moja,” amesema.
Ameongeza kuwa taarifa zote za changamoto ya malazi chuoni hapo hukusanywa kuanzia ngazi ya chini ikiwemo serikali ya wanafunzi, viongozi, wasimamizi na walezi wa mabweni ambao pia hawana taarifa hizo.
Mdami amesema chuo hicho kinajitosheleza katika eneo hilo, na litafanya ukarabati kwenye baadhi ya majengo ambayo yalikuwa yakitumika kama ofisi za wakufunzi ili yatumike kama mabweni ya akiba ikiwa changamoto hii itajitokeza kweli.
Mbali na hayo amesema pia chuo hicho kitaanza kufanya ukaguzi kwenye mabweni yake ili kuwabaini wanaolala zaidi ya mmoja kwa kuwa jambo hilo ni kinyume cha utaratibu wa chuo hicho.
