WAKATI Klabu ya Mbeya City ikiwa katika mazungumzo ya kupata saini ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Awesu Ally Awesu, uongozi wa Kenya Police ya Kenya, umeingilia kati dili hilo kwa ajili ya kumpata nyota huyo kwa mkopo wa miezi sita.
Kenya Police ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Kenya msimu uliopita, wamefungua mazungumzo hayo kwa ajili ya kupata saini yake kwa mkopo, huku Mbeya City ikipambana kuhakikisha inakamilisha pia dili hilo kwa wakati kabla ya kupigwa bao.
Chanzo kutoka Mbeya City, kimeliambia Mwanaspoti Awesu bado ni mchezaji anayehitajika na benchi la ufundi la timu hiyo kwa lengo la kuongezea nguvu eneo la ushambuliaji, ingawa wamepata taarifa pia klabu mbalimbali zimeanza kuingilia kati.
“Bado uongozi unapambana kwa ajili ya kukamilisha dili lake, ila ushindani umekuwa ni mkubwa kwa sababu tumesikia timu nyingine pia zimeanza mazungumzo na waajiri wake Simba, sisi tutapambana tuone mwisho itakuwaje,” kilisema chanzo hicho.
Wakati mabosi wa Mbeya City wakipambana kukamilisha dili hilo, taarifa zinaeleza Kenya Police imetuma wawakilishi wake kwa ajili ya kufuatilia upatikanaji wa nyota huyo, ingawa uamuzi wa mwisho utabakia kwa mchezaji kuamua atakapokwenda.
Kenya Police iliyotwaa ubingwa wa Kenya msimu wa 2024-2025, ikiwa chini ya Kocha, Mrundi Etienne Ndayiragije, ambaye kwa sasa anaifundisha TRA United, inamhitaji kiungo huyo kwa ajili ya kuongeza makali katika eneo la kiungo mshambuliaji.
Kocha huyo aliipa Kenya Police ubingwa huo ukiwa ni wa kwanza kwa kikosi hicho katika historia tangu kilipopanda daraja mwaka 2021, hivyo, kuzima utawala wa Gor Mahia iliyochukua mara mbili mfululizo kuanzia msimu wa 2022-2023 na 2023-2024.
Awesu aliyejiunga na Simba Julai 16, 2024, baada ya kuachana na KMC, ameshindwa kupenya kikosi cha kwanza kutokana na ushindani, jambo linalosababisha kutolewa kwa mkopo, huku akiwahi pia kuzichezea Klabu za Kagera Sugar, Azam na Mwadui.
