Wawili wafariki kwenye kampeni Uganda, yumo mwanamke aliyekuwa akigombania fulana

Kampala. Aliyekuwa mlinzi wa Mgombea urais wa upinzani kutoka Chama cha (NUP), Robert Gyahulanyi maarufu Bobi Wine amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.

Taarifa za kifo cha mlinzi huyo imetolewa na kupitia mitandao ya kijamii ya Bobi Wine ikieleza masikitiko ya kifo cha mlinzi huyo aliyefahamika kwa jina la Fransis Kalibala, akidai kuwa aligongwa na gari la jeshi kwenye eneo la Busega.

Amedai kuwa gari hilo lilikuwa limesimama njiani kuzuia msafara wa mgombea huyo usipitie kuingia kwenye mji huo kwa ajili ya kampeni.

Taarifa ambayo imekanushwa na  Msemaji wa Jeshi la Uganda, Brigedia Falvia Byekwaso na kueleza kuwa Fransis alifariki baada ya kuanguka  kwenye gari na si kugongwa kama alivyoeleza Bobi Wine.

“Fransis hakugongwa na gari la Jeshi UPDF ila alianguka kutoka kwenye gari namba UBF 850Z,” amesema Byekwaso.

Katika tukio lingine imeelezwa kuwa mwanamke mmoja nchini humo amefariki dunia katika mkanyagano katika kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika wiki hii nchini humo.

Tukio hilo limetokea katika kampeni za chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) kinachoongozwa na  Yoweri Museveni anayetetea nafasi hiyo.

Mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Rose Ajiko amefariki katika Wilaya ya Soroti  baada ya kukanyagwa na wenzake alipokuwa akigombania fursa ya kupata fulana ya mgombea urais wa chama hicho, Yoweri Museveni ambaye pia ni rais wa sasa wa taifa hilo.

Imeelezwa kuwa, Rose (28) alikuwa miongoni mwa wafuasi waliokusanyika kutoka eneo la Kamuda alifariki Januari 10, 2026 wakati mkutano wa mgombea ubunge Patrick Aeku baada ya kuanguka chini na kukanyagwa na wafuasi wengine wakati wa ugawaji wa fulana hizo.

Matukio hayo yameilazimu Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kusitisha kampeni katika miji kadhaa ikiwemo Mbarara, Masaka, Wakiso, jinja, Kalungu, Kazo na Tororo huku ikielezwa kuwa kuna viashiria vya uwepo wa virusi vya Uviko-19 kwenye maeneo hayo.

Jambo ambalo limeonekana kutiliwa shaka na wanasiasa wa taifa hilo wakihoji kwa nini maeneo yaliyozuiwa ni yale ambayo mgombea urais wa NRM, Yoweri Museveni ameshafanya kampeni na ilikuwa zamu ya Bobi Wine.