Bobi Wine atishia maandamamo akihujumiwa, aagiza kulinda kura Alhamisi

Uganda. Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Chama cha National Unity Platform (NUP) Robert Gyahulanyi  maarufu Bobi Wine ameonya kuwa atatoa wito wa maandamano nchini Uganda iwapo Rais Yoweri Museveni atahujumu uchaguzi wa urais unaofanyika  wiki hii.

Uchaguzi Mkuu nchini humo unatarajiwa kufanyika Alhamisi wiki hii huku zaidi ya Waganda milioni 20 wakijiandaa kupiga kura,

Bobi Wine anayegombea urais kwa mara ya pili nchini Uganda, katika taarifa yake ya leo Jumanne Januari 13, 2026, ametoa wito kwa upinzani nchini  kulinda kura zao na iwapo kutatokea kuibwa kura ataitisha maandamano nchi nzima.

“Tumesema mara nyingi kwamba iwapo Jenerali Museveni atahujumu uchaguzi, tutatoa wito wa maandamano,” Wine aliiambia AFP

Museveni, mwenye miaka 81, anapewa nafasi kubwa ya kushinda na kuendelea kutawala ikiwa ni takribani miongo minne.

Makundi ya kutetea haki za binadamu, yakiwemo Umoja wa Mataifa na Amnesty International, yamezituhumu mamlaka za Uganda kwa kukandamiza upinzani kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu nchini humo, yakitaja kukamatwa wafuasi wa Wine.

Wine, mwenye umri wa miaka 43, anawania urais kwa mara ya pili baada ya kampeni yake ya mwaka 2021 kugubikwa na ukandamizaji wa kikatili na madai ya udanganyifu.

Wine amesisitiza kuwa upinzani unaendelea kupata uungwaji mkono mkubwa wa wananchi, lakini akaibua wasiwasi kuhusu iwapo madaraka yangehamishwa kwa amani.

 “Je, tunachukua madaraka? Hilo ni swali kwa wananchi, jumuiya ya kimataifa, na kwa Jenerali Museveni, ambaye anashikilia madaraka kwa kutumia bunduki,” amehoji.

Wine amesema maandamano yanaweza kusababisha vurugu zaidi, lakini kutokutumia nguvu bado ni jambo la msingi, akiongeza kuwa tawala za kikandamizaji huondolewa kwa maandamano.

Umati mkubwa wa vijana umeendelea kujitokeza kumuunga mkono Wine mjini Kampala, jambo linaloakisi mwamko wa vijana katika ushiriki wa  demokrasia.