Dalili njema mafuta kushuka bei 2026

Dar es Salaam. Wamiliki wa magari nchini Tanzania wanaweza kushuhudia unafuu wa bei za mafuta mwaka 2026, kufuatia utabiri wa soko la dunia unaoonesha uwezekano wa ongezeko la uzalishaji wa mafuta ghafi na kushuka kwa bei ya nishati hiyo.

Tafiti za masoko ya kimataifa zinaonesha kuwa, bei za mafuta ghafi huenda zikashuka mwaka 2026, huku makadirio yakionesha wastani wa bei ya kuwa kati ya Dola 60 hadi Dola 65 za Marekani kwa pipa, na baadhi ya wachambuzi wakitabiri kushuka hadi Dola 50 za Marekani iwapo ziada ya uzalishaji itaongezeka zaidi.

Hali hii inatokea wakati uzalishaji wa mafuta ukiendelea kuongezeka kutoka kwa wazalishaji wakubwa na nchi kama Venezuela kurejea tena kwenye soko la kimataifa baada ya muda mrefu, jambo ambalo wachambuzi wanasema litaongeza kiasi cha mafuta duniani.

Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Mafuta Tanzania (TAPSOA), Tino Mmasi amesema kuna sababu kubwa ya kuamini kuwa bei za mafuta nchini zitashuka mwaka huu.

“Ni kweli bei zitashuka katika miezi ijayo ya 2026 kwa sababu tunategemea sana bei za dunia,” amesema Mmasi, akibainisha nguvu ya Shilingi ya Tanzania kuanzia mwishoni mwa 2025 hadi 2026 imechangia kupunguza gharama za mafuta yanayoingizwa nchini.

Alikumbusha kuwa, katika miezi mitatu hadi minne iliyopita, bei za mafuta nchini zilipungua kwa kiasi kikubwa baada ya shilingi kuimarika dhidi ya Dola ya Marekani.

Kwa mujibu wa bei za juu zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) Jumatano, Januari 7, 2026, petroli iliyopokewa kupitia bandari ya Dar es Salaam inauzwa kwa Sh2,778 kwa lita  ikilinganishwa na Sh2,749  Desemba.

Dizeli imeshuka hadi Sh2,726 kwa lita kutoka Sh2,779, huku mafuta ya taa (kerosene) yakipanda hadi Sh2,763 kutoka Sh2,653.

Hata hivyo, Mmasi alitoa angalizo kuwa mabadiliko ya bei za mafuta ghafi duniani hayataonekana mara moja kwenye bei za rejareja, kwa sababu mafuta huagizwa miezi miwili hadi mitatu kabla.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kampuni za Uuzaji Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alikubaliana na mtazamo huo akisema hali ya uzalishaji mkubwa wa mafuta duniani ilianza kabla ya matukio ya sasa.

“Hata kabla ya matukio ya sasa duniani, masuala ya Venezuela na masoko mengine tayari yalionesha dalili za kushuka kwa bei hadi Dola 50 kwa pipa mwaka huu,” amesema Mgaya.

Ameeleza kuwa, Venezuela ambayo awali ilikuwa ikizalisha chini ya uwezo wake, sasa inaongeza uzalishaji chini ya masharti mapya, jambo litakaloongeza mafuta sokoni na kushusha bei zaidi.

Mgaya alitabiri kipindi kirefu cha unafuu wa bei endapo hali ya uzalishaji kupita kiasi itaendelea.

“Kwa kuwa, Tanzania tunaagiza mafuta yote kutoka nje na bei ya dunia inachangia sehemu kubwa ya gharama tunayolipa, bei inaposhuka kimataifa, mafuta yanakuwa nafuu pia hapa nchini,” amesema.

Kwa wamiliki wa magari, kushuka kwa bei za mafuta duniani kutamaanisha kupungua kwa matumizi ya mafuta hasa petroli na dizeli.

Watoa huduma za usafirishaji, ambao wamekuwa wakipambana na gharama kubwa za uendeshaji kutokana na mabadiliko ya bei za mafuta, watakuwa miongoni mwa wanaonufaika zaidi.

Mafuta ya bei nafuu pia yanaweza kusaidia kupunguza kasi ya mfumuko wa bei, hasa kwenye bidhaa na huduma zinazohusiana na gharama za usafiri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi na Maendeleo ya Ujasiriamali (IMED), Dk Donath Olomi amesema utegemezi mkubwa wa Tanzania kwa mafuta ya kuagizwa kutoka nje unaendelea kuathiri gharama za sekta nyingi za kiuchumi.

“Tanzania inaagiza kiasi kikubwa cha bidhaa za mafuta, jambo linaloathiri moja kwa moja gharama za karibu kila kitu,” amesema.

Amefafanua kuwa, mafuta ni kiungo muhimu si tu kwenye usafirishaji bali pia katika uzalishaji viwandani, kilimo, uchakataji wa malighafi na biashara.

“Iwapo bei za mafuta zitashuka, unafuu hautaishia kwenye usafiri pekee. Utapunguza gharama za uzalishaji, kurahisisha shughuli za kilimo, kupunguza gharama za malighafi na kuongeza ufanisi wa biashara katika sekta mbalimbali,” amesema Dk Olomi.

Ameongeza kuwa, kupungua kwa bei za mafuta kwa kipindi kirefu kunaweza kusaidia ukuaji wa uchumi kwa kuboresha faida za kampuni, kuongeza kipato cha kaya na kuchochea matumizi ya wananchi.

“Kwa jumla, unaweza kusema kushuka kwa bei za mafuta kuna uwezo mkubwa wa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi,” amesema.

Mtazamo huu unaendana na tathmini ya hivi karibuni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo Baada ya Kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kilichofanyika Januari 7, 2026, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema bei za mafuta ghafi duniani zilishuka hadi kati ya Dola 62 na 65 za Marekani kwa pipa, katika robo ya nne ya mwaka 2025 na zinatarajiwa kubaki katika kiwango hicho katika robo inayofuata kutokana na uzalishaji mkubwa na mahitaji madogo duniani.

“Mwelekeo huu utaendelea kutoa unafuu kwa mfumuko wa bei nchini Tanzania, mahitaji ya fedha za kigeni na uthabiti wa thamani ya shilingi, kwani sasa mafuta ya kuagizwa kutoka nje yanachukua takriban asilimia 17 ya bidhaa zinazoingizwa,” amesema gavana katika taarifa yake.