Dodoma/Moshi. Wakati utoaji wa haki kwenye mahakama nchini ukilalamikiwa, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju ametaja mambo manane anayoyataka yapatiwe ufumbuzi ili kuufanya mhimili huo kuwa huru na usioingiliwa katika utoaji haki.
Miongoni mwa mambo aliyoyataja Jaji Masaju ni usalama katika ajira za majaji na mahakimu, maboresho ya mishahara na stahiki zao, urahisi wa kufikia huduma za mahakama na ufanisi kwa wakati.
Mambo mengine ni kuwepo kwa mfuko mkuu wa mahakama, uadilifu na uwazi, upatikanaji wa fedha za kutosha na kuondolewa ulipwaji wa stahiki na posho ikiwemo malipo ya kustaafu kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, suala ambalo amesema ni kuvunja Katiba.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), uliofanyika leo Junuari 13, 2026 katika viwanja vya makao makuu ya Mahakama jijini Dodoma. Picha na Ikulu
Kwa muda mrefu kumekuwepo na malalamiko miongoni mwa wananchi kuhusu utendaji wa mahakama nchini, huku kauli za kuutaka mhimili huo kutoa zikisikika kila mara.
Hata hivyo, wakati Jaji Masaju akieleza hayo leo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, wanasheria wameshauri jambo tofauti la kuufanya ili mhimili huo uwe na uhuru.
Wamesema ni lazima iwepo Katiba inayolinda ukuu wa mahakama na uwepo wa utawala wa sheria.
Akifafanua hilo, Wakili Aloyce Komba kutoka kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza ya jijini Dar es Salaam, alikwenda mbali na kusema ili mahakama iwe huru ni lazima yenyewe ijijue kuwa inapaswa kuwa huru kuanzia majaji, mahakimu na anayeongoza mhimili.
“Wakitambua ibara ya 107A na wakaizingatia, maamuzi yake hayataingiliwa na Bunge ambalo kazi yake ni kutunga sheria wala Serikali ambayo kazi yake ni kutekeleza sheria. Chombo cha mwisho kwenye utoaji haki ni Mahakama,” alisema.
Wakili mwingine ambaye hakutaka kutajwa, alieleza namna mahakama inavyoingiliwa na mihimili mingine wakitolea mfano wa suala la mgombea binafsi, ambapo Mchungaji Christopher Mtikila alishinda kesi ya Kikatiba mbele ya Jaji Kahwa Lugangikira akatamka ni haki.
Badala ya kukata rufaa, mwaka 1994 Serikali iliwasilisha bungeni mabadiliko ya 11 ya Katiba na katika ibara ya 39 na 67 waliweka sharti kuwa kugombea nafasi za kuchaguliwa ni lazima mgombea atokane na chama cha siasa.
Jambo hilo liliwahi kuzungumzwa na Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta alipostaafu mwaka 2007, kuwa Bunge lina mipaka katika utungaji sheria.
Alieleza hayo alipokuwa akijibu swali kuhusu mtazamo wake juu ya vitendo vilivyofanywa na mihimili mingine kufuta uamuzi wa Mahakama na kutotekeleza hukumu zake na badala yake kutunga sheria mpya au kuibadili Katiba ya nchi.
Jaji Samatta alisema “Bunge lina kazi ya kutunga sheria na linachotakiwa kufanya ni kufanya mabadiliko tu ya sheria kwa kadri hukumu ya Mahakama ilivyoelekeza na si kufuta uamuzi wa Mahakama,” kauli iliyokoleza haja ya uhuru wa mahakama.
Kauli ya jana ya Jaji Masaju ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ni kama imetonesha kidonda cha wanasheria, wanaharakati na wananchi wanaoiona mahakama si huru katika maamuzi yake.
Baadhi ya mahakimu na majaji walioshiriki mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), uliofanyika leo Junuari 13, 2026 katika viwanja vya makao makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Kauli hiyo imekuwa wakati Katiba ya Tanzania Ibara ya 107A (1) inasema mamlaka ya utoaji haki Tanzania itakuwa mikononi mwa Idara ya Mahakama na kwa hiyo hakuna chombo cha Serikali wala Bunge kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.
Vilevile, Ibara ya 107B 107B inasisitiza kuwa katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.
Pamoja na Katiba kuufanya mhimili huo kuwa huru, bado kuna hisia kuwa baadhi ya maamuzi inayoyatoa yanayojenga hisia kuwa yanaegemea upande wa Serikali.
Mbali na kilio cha utendaji haki, suala la utendaji wa mahakama, liliwahi kumulikwa pia na Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia na kuwasilisha ripoti yake kwake Julai 2023, ambayo ilielezea namna ya kuwepo ucheleweshaji wa mashauri mahakamani.
“Kumekuwepo na malalamiko kuhusu ucheleweshaji wa kusikiliza mashauri katika Mahakama Kuu. Tume ilibaini kuwa kuna mashauri mengi zaidi ya 1,000 ambayo yamefungwa na yanasubiri kusikilizwa na Mahakama Kuu,” ilisema Tume.
Akitoa hotuba wakati akihutubia kwenye mkutano Mkuu wa TMJA uliofanyika jijini Dodoma jana ambao mgeni rasmi alikuwa Rais Samia, Jaji Mkuu Masaju alitaja mambo hayo akitaka yafanyike ili kuwezesha mhimili huo kuwa huru na maamuzi yake yasiingiliwe.
Jaji Masaju alisema mambo hayo yakifanyika, anaamini majaji na mahakimu watatoa haki bila upendeleo, woga, rushwa wala shinikizo kutoka mahali pengine.
Mkutano huo uliwakutanisha zaidi ya majaji na mahakimu 1,200 kati ya wanachama 1,700 ukiwa na kaulimbiu ya Jukumu la Mahakama Huru katika utoaji haki.
Jaji Masaju alisema: “Mheshimiwa Rais, pensheni za majaji na mahakimu kulipwa na mtendaji mkuu wa mahakama ni kuvunja Katiba, rudisheni malipo hayo Hazina,” alisema.
Akifafanua, Masaju alisisitiza umuhimu wa kikatiba wa uhuru wa Mahakama, akibainisha mhimili huo una mamlaka ya mwisho katika utoaji haki kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa kuwa mahakama ni sehemu ya Serikali na dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, inapaswa kuwa huru isiingiliwe na mihimili mingine inayounda Serikali na dola ya Jamhuri,” amesema.
Katika hiyo, Jaji Mkuu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan “kwa dhamira ya dhati ya kuimarisha uhuru wa Mahakama”, akisema hatua na kauli za zake zimeonyesha wazi heshima kwa mhimili huo muhimu wa dola.
Alisema kuna baadhi ya watendaji wanakaa mahali na kufanya mambo aliyosema ni ya ajabu na yasiyoweza kusaidia haki za watoa haki.
“Mtu anayeshindwa kuwajali na kuwathamini majaji na mahakimu na hata posho za jaji mkuu kucheleweshwa kwa zaidi ya miezi sita, hii siyo sawa,” alisema.
Mbali na stahiki hizo, Jaji Masaju alisema majaji na mahakimu wanahitaji kuwa na makazi bora na kwenye maeneo yenye utulivu na usalama kwa sababu maisha yao yanaweza kuwa ndani ya vishawishi kutokana na kuchanganyika.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), uliofanyika leo Junuari 13, 2026 katika viwanja vya makao makuu ya Mahakama jijini Dodoma. Picha na Ikulu
Alisema mazingira ya watumishi hao wakati mwingine ni ya hatari, hasa wanapotakiwa kutoa hukumu kwa watu ambao, wamewapangisha kwenye nyumba na badala yake wanajikuta wanashindwa kufanya maamuzi sahihi.
“Maisha yetu ni ya kujitenga na jamii, kiasi ambacho hupelekaa msongo wa mawazo na sonona kwa kukosa mazingira bora ya kuishi na hali za kiuchumi kuwa duni,” amesema.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amesema Mahakama nchini zitaanza kuandika hukumu kwa lugha ya Kiswahili mara baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kukamilisha tafsiri ya matoleo ya kisheria kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakapokuwa amekamilisha tafasiri ya matoleo ya kisheria kwa lugha ya Kiswahili, tutaanza pia kuandika hukumu kwa Kiswahili. Nimeambiwa yuko katika hatua za mwishoni, na sheria tayari ilishatungwa inayosema lugha ya Mahakama itakuwa ni ya Kiswahili,” amesema Masaju.
Amesema matumizi ya Kiswahili katika nyaraka na hukumu za Mahakama yatasaidia kuongeza uwazi, kuimarisha imani ya wananchi kwa mfumo wa sheria na kurahisisha utekelezaji wa maamuzi ya mahakama.
Jambo jingine ambalo Jaji Mkuu Masaju amesema wanakusudia kufanyia marekebisho ya muundo wa usimamizi wa Kamati za maadili za maofisa wa mahakama kwa kuwaondoa Wakuu wa Mikoa (RC), Wakuu wa Wilaya (DC) na Makatibu tawala katika muundo.
Amesema lengo la marekebisho hayo ni kuimarisha uhuru wa mahakama kwa kuhakikisha usimamizi wa nidhamu unafanyika ndani ya Mahakama yenyewe kwani kwa sasa wakuu wa mikoa na wilaya ni wanasiasa, akisisitiza uamuzi huo umechelewa kufanyika.
Katika hatua nyingine, Jaji Masaju ameitaka Serikali kufanya kubadili mfumo wa usuluhishi wa kesi za migogoro ya ardhi ili zihamie mahakamani kwa kuwa ndiko kwenye utoaji wa haki badala ya mabaraza ya ardhi ambayo yanaichelewesha.
Alisema kuwepo na mabadiliko ya sheria na mifumo kwani mambo mengi yamepitwa na wakati na hayaendani na maisha ya sasa.
“Katiba inasema haki zote zitapatikana kupitia chombo cha Mahakama, leo hii kuna mabaraza ya ardhi ya kata na wilaya badala ya mfumo wa kimahakama, hiyo siyo sahihi,” alisema Jaji mkuu.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema uwepo wa mahakama huru yenye uwezo na uadilifu ni nguzo muhimu ya utawala bora na msingi wa upatikanaji wa haki.
Kutokana na hilo, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuulinda na kuuheshimu uhuru wa mahakama.
Hata hivyo, ametoa angalizo kwamba uhuru huo hauna budi kwenda sambamba na uwajibikaji, uadilifu, nidhamu, utii wa sheria na uzalendo kwa Taifa.
Kabla ya kueleza hayo, Mkuu huyo wa nchi, amesema hakuna Taifa linaloweza kuwa na maendeleo endelevu na ustawi wa watu wake bila usimamizi mzuri wa haki.
“Watanzania wana matumaini makubwa na nyinyi, wangependa kuona mahakama inayosimamia haki kwa uwazi kwa kuzingatia misingi ya kikatiba sheria na utu.
“Huko mahabusu kuna mtu anafungwa kwa kesi ya kubambikiwa, sasa nini kimetokea mahakamani hadi mtu anafungwa kwa kesi ya kubambikiwa… Akitoka anasema sikuwa na kesi nilibambikiwa tu,” amesema Rais Samia.
