Dar es Salaam. Wakati muhula wa masomo wa mwaka 2026 ukianza rasmi leo, baadhi ya wanafunzi wamekutana na changamoto kubwa ya usafiri hususan kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali.
Katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli na vituo vidogo Manzese na Shekilango jana kulikuwa na abiria wengi wakihaha kusaka usafiri wengi wakiwa ni wazazi walioambana na watoto wao kuwasindikiza.
Wakiwa na mizigo yao, wapo waliokuwa wakitoka Manzese hadi Shekilango kwa bodaboda na wengine wakilazimika kwenda Stendi ya Magufuli kutafuta usafiri hata ule wa kuungaunga ambao nao ulikuwa mgumu.
Wapo ambao hadi inafika saa 10 jioni ya jana walikuwa hawajapata usafiri hivyo kwa vyovyote vile, hawaweza kuhudhuria siku ya kwanza shuleni ambapo muhula unaanza. Baadhi ya shule zilifungulia Januari 5.
Licha ya ugumu wa usafiri kwenda mikoa mbalimbali nchini hususan Morogoro, Mbeya, Dodoma, Singida, mikoa ya nyanda za juu Kusini kama Mbeya, Iringa, Njombe na ile ya kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga, wimbi la kupanda holela kwa nauli likaibuka.
Katikati ya adha hiyo ya usafiri, upande mwingine imekuwa ni kicheko kwa wasafirishaji ambao siku za karibuni walikuwa hawana abiria na kuwalazimu kupunguza mabasi barabarani.
Kutokana na tatizo hilo, baadhi ya shule zimekuwa na utaratibu wa kukodi mabasi ambayo huwabeba wanafunzi kwa pamoja na kuwapelaka shuleni.
Utaratibu huo unaelezwa kupunguza adha kwa wanafunzi wenyewe wawapo safarini kwani wengi hawasafiri na simu lakini kwenye mabasi maalumu wanakuwa na viongozi wa shule.
Mbali na wanafunzi waliokuwa wakihenya na wazazi wao, kulikuwa na abiria wa kawaida ambao kutokana na wimbi kubwa la wanafunzi kurejea shule, nao walijikutana wakihaha kusafa usafiri.
Mwananchi iliyopiga kambi maeneo hayo kuanzia asubuhi ya jana hadi jioni, ilishuhudia hekaheka za hapa na pale kwa abiria hao wakiwemo wengine ambao ni wanafunzi wanaokwenda kuanza kidato kwanza.
Ugumu huo wa usafiri upo pia kwa treni ya kisasa ya SGR kwenda Morogoro na Dodoma, kuanzia Ijumaa hadi leo (jana), tiketi hazipatikana kwani zilikuwa zimekatwa mapema.
Kwa nyakati tofauti, baadhi ya abiria walipozungumza na Mwananchi wamedai adha hiyo ya usafiri imewachanganya kiasi cha kuwaletea msongo wa mawazo huku wengi wao wakikosa matumaini ya kupata usafiri kutokana na uhaba wa mabasi yanayoenda hadi maeneo wanayohitaji.
Wamedai kulazimika kusubiri bila uhakika wa safari, jambo linalowaathiri watoto ambao wanatakiwa kuwahi shuleni kwa wakati ili kuanza masomo wengi wakijutia na kudai wangejua wangesafiri mapema.
Baadhi ya wazazi wameeleza ukosefu wa vipato vya uhakika pamoja na matatizo ya kijamii ni miongoni mwa sababu zinazowafanya kushindwa kuwasafirisha mapema watoto wao kurejea shuleni, hali inayowalazimu kukumbana na adha ya usafiri.
Pia, baadhi yao wamedai Januari ni mwezi wenye majukumu mengi ya kifamilia na kiuchumi, hali inayozidi kuathiri uwezo wao wa kugharamia usafiri kwa wakati.
Aidha, kuna hoja kwamba wengine wanapokwenda wanazingatia matakwa ya shule zinafunguliwa lini na kumuwamisha mapema mtoto hakuna sehemu ya kufikia, lakini kama kuna ndugu wangeweza kuwasafirisha mapema kwenda mkoa husika.
Gabriel Moshi, mzazi anayehangaika kumsafirisha mtoto wake kwenda Morogoro, amesema wengi wao hawana vipato vya uhakika bali hutegemea vibarua na michongo ya hapa na pale.
Amesema hali hiyo inawafanya washindwe kupanga mapema safari za watoto wao.
“Ni rahisi kuuliza kwa nini hatuwapeleki mapema, lakini ukweli ni kwamba vipato vyetu si vya uhakika. Wengi tunaishi kwa kusikilizia tupate lini. Ukipata ndipo utumie, ndiyo maana tunachelewa kuwarejesha watoto shuleni,” amesema Moshi.
Ameongeza wazazi hawapendi kukumbana na usumbufu wa kusaka usafiri chini ya jua kali, lakini hali ya kiuchumi inawalazimu kuvumilia.
Naye Sofia Lema anayesafirisha mtoto kwenda mkoani Kilimanjaro, amesema mbali na mabasi yamejaa kwa siku kadhaa, alipitia msiba wa kufiwa na ndugu wa karibu uliomuingiza katika gharama kubwa zisizotarajiwa.
“Nilipata msiba na nililazimika kutumia fedha nyingi, hali iliyoniyumbisha kiuchumi. Ndiyo maana sikuweza kumpeleka mtoto mapema shuleni.
“Kwa sasa nimepata fedha na ninaendelea kuhangaika kutafuta usafiri, naamini nitafanikiwa,” amesema Lema.
Mzazi mwingine, Agnes Lucky anayempeleka mwanafunzi Dodoma amesema alikosa tiketi ya SGR, akahisi kwenye basi atapata kirahisi.
“Kwenye kila basi zuri la Dodoma nilipojaribu kuangalia tiketi naambiwa nimejaa, kama ningekuwa na kipato cha uhakika ningemkatia mwanangu tiketi mapema,” amesema.
Mmoja wa mzazi ambaye anasomesha mtoto moja ya shule Bukoba mkoani Kagera anayeishi Dar es Salaam anasema shule yao huwa kuna utaratibu wa kuwatoa watoto shule na kuwarejesha.
“Wazazi wanaweza kuandaa utaratibu wanawa wanakodi mabasi yanawachukua watoto kwa pamoja na ni salama zaidi kwa usalama wao. Kwenye basi kunakuwa na viongozi wa shule. Kwa hiyo walezi na wazazi wafikirie utaratibu huu ambao ni mzuri kama ambavyo sisi tunafanya kwa shule yetu,” amesema mzazi huyo aliyeomba hifadhi ya jina.
Kicheko kwa wasafirishaji
Katikati ya adha hiyo ya usafiri, upande mwingine umekuwa ni fursa kwa wasafirishaji ambao hakuna basi lililokuwa likisafiri tupu na hata zile Coaster zilichangamkia fursa hiyo.
Mathalani nauli ya Dar es Salaam kwenda Morogoro ni Sh10,000 lakini kwa hali ilivyokuwa nauli ilipanda hadi kufikia Sh15,000 hadi Sh20,000.
Mmoja wa wamiliki wa mabasi ya mikoani aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema: “Unajua tulikuwa na hali ngumu ya abiria, baada ya watu kusafiri sana kabla ya Desemba 9, hapo katikati abiria walikata, sasa kwa saizi tunafidia na kwa kweli tunapiga hela kwelikweli.”
“Kwa siku za karibuni hali imerejea vizuri, tunakwenda mikoani na kurudi Dar es Salaam tukiwa na abiria wa kutosha na inatupunguzia gharama za uendeshaji kwani ukikosa abiria unakosa kununua mafuta na kubaki na faida,” ameongeza.
Mbali na changamoto ya upatikanaji wa usafiri, baadhi ya abiria katika Stendi ya Magufuli wamelalamikia kupandishwa kiholela kwa nauli, hali inayoongeza ugumu wa safari kwao.
Nelia Rugaza amesema tiketi zinauzwa kwa bei tofauti licha ya safari kuwa ileile.
Ameeleza kuwa, baadhi ya abiria wanashawishiwa kulipa fedha zaidi na madalali kwa kisingizio cha uhaba wa mabasi.
“Wapo wanaokubali kulipa nauli kubwa ili wasichelewe kufika wanakokwenda. Sisi ambao hatuna uwezo huo tunaendelea kusota stendi, kwani kila tunapofika kwenye kampuni tunaambiwa mabasi yamejaa,” amesema Rugaza.
Kwa upande wake, Omary Mrisho amesema amesubiri usafiri wa kwenda Ifakara kwa zaidi ya saa nne bila mafanikio.
Amesema alifika stendi saa 4 asubuhi na hadi saa 8:22 mchana hakuwa amepata usafiri, huku akidaiwa kutoa Sh65,000 ili atafutiwe basi, wakati nauli halali ni Sh25,000.
“Ikifika saa 11 jioni bila kupata usafiri, nitarudi nilikotoka,” amesema.
Muddy Limbu, aliyekuwa akisafiri na mkewe pamoja na mtoto mchanga, amesema amekuwa stendi tangu saa 5 asubuhi akitarajia kupata basi la kwenda Maswa bila mafanikio.
Amedai dalali mmoja alimtaka kulipa Sh90,000, ilhali nauli ya kawaida ya safari ya Dar es Salaam–Maswa ni kati ya Sh65,000 hadi Sh70,000.
Naomi Msangi, aliyekuwa akisafiri kwenda Mwanza akiwa na kijana wake, amesema tayari ana tiketi na anachosubiri ni basi kufika ili kuanza safari.
Mmoja wa madereva ambaye aliomba kutotajwa jina amesema changamoto ya usafiri ipo kwa abiria wanaotarajia kukata tiketi na kusafiri siku hiyo hiyo.
Amesema abiria waliokata tiketi mapema huenda wakachelewa kwa dakika chache tu kutokana na sababu za kiufundi, lakini kwa wale wasio na tiketi, kupata usafiri leo (jana) ni changamoto kubwa.
“Wale walio’book’ mapema wanaweza kuchelewa kwa dakika kadhaa tu, lakini kwa wasio na tiketi, kupata usafiri leo (jana) ni ngumu,” amesema dereva huyo.
Mdau mwingine wa usafirishaji aliyejitambulisha kwa jina moja la Elly amesema hali ni mbaya zaidi kwa mabasi ya Morogoro, ambapo abiria wengi hukata tiketi siku ya safari.
“Leo (jana) mabasi ni machache na abiria ni wengi. Wale wenye utaratibu wa kukata tiketi mapema hawana shida, lakini wanaokata siku hiyo hiyo na kusafiri siku hiyo hiyo wanapata ugumu mkubwa. Huenda wakapata Coster, lakini kwa mabasi makubwa ni vigumu,” amesema Elly.
Akizungumza kuhusu malalamiko ya kupandishwa nauli, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra), Kituo Kikuu cha Mabasi Magufuli Dar es Salaam, Rukia Kibwana amesema mamlaka hiyo huchukua hatua pale malalamiko yanapowasilishwa.
“Kuna mawakala wanaosaidia abiria kupata usafiri. Kama hakuna malalamiko, hata maofisa wa Latra wakifika huwa hakuna ushahidi,” amesema.
Ameeleza kuwa iwapo abiria atalalamika, basi linalobainika kupandisha nauli kinyume cha sheria hufunguliwa kesi ya wizi na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufikishwa polisi.
Amesema kupandisha nauli kwenye tiketi za kielektroniki ni kosa, na anayekutwa akifanya hivyo huchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.
