Mufindi. Madiwani katika halmashauri za Wilaya ya Mufindi na Mji Mafinga wametakiwa kutumia vizuri mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo), kuimarisha uwajibikaji, ubunifu na ufanisi wa uongozi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo Jumanne Januari 13, 2026, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Reuben Chongolo, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Dk Linda Salekwa amesema kupitia mafunzo hayo, madiwani watapata uelewa mpana wa majukumu na mipaka ya madaraka yao kwenye usimamizi wa rasilimali za umma, mipango na bajeti kwenye halmashauri zao.
Chongolo amesema wananchi wanatarajia kuona matokeo chanya ya uongozi wao kupitia kutoa huduma bora katika maeneo yao, hivyo mafunzo hayo yatawaletea mabadiliko ya kiutendaji kutokana na kubadilika kwa nyakati.
“Niwasihi madiwani tujifunze kusikiliza ndipo tufanye uamuzi, badala yake tusiendelee na mazoea ya zamani mliyokuwa nayo kwa sababu nyakati zimebadilika, wananchi wanaangalia na wanatarajia kuona matokeo chanya,” amesema Chongolo.
Kwa upande wake, mkufunzi kutoka Hombolo, Petro Nziku amesema mafunzo hayo ni elekezi kwa ajili ya madiwani, lengo likiwa kuwapa uelewa kuhusiana na majukumu na mipaka yao ya kiutendaji.
“Tumewapa nyenzo muhimu katika mada mbalimbali ikiwemo ya uongozi na utawala bora, sheria za serikali za mitaa, wajibu na stahiki zao kama madiwani, usimamizi wa fedha, mpango wa maendeleo na bajeti, maadili ya madiwani pamoja na kuwasimamia watumishi,”amesema.
Pia, Nziku amewaasa madiwani kusikiliza kwa umakini kwa sababu Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya madiwani kupata mafunzo hayo.
“Mafunzo haya yatawawezesha kufanya kazi zao kwa tija, lengo kubwa ni kufanikisha utoaji wa huduma kwa wananchi ili kutoa tabasamu kwa wananchi,” amesema mkufunzi huyo.
Mwenyekiti wa Wilaya ya Mufindi, Castory Masangula amesema mafunzo hayo yatawasaidia madiwani katika utekelezaji wa majukumu kwenye kata zao ukizingatia wengi wao ni wapya na hawajui namna ya utendaji kazi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza kutolewa Januari 12, 2026 na yanatarajiwa kumalizika Januari 14.