Magari 21 yazuiwa kubeba wanafunzi Kilimanjaro

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limeyazuia magari 21 ya shule kuendelea na shughuli za usafirishaji wa wanafunzi, baada ya kubainika kuwa ni mabovu na hayako katika hali salama ya kusafirisha wanafunzi.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ukaguzi maalumu wa magari ya shule uliofanyika kuanzia Januari 9 hadi Januari 12, 2026 katika wilaya zote za mkoa huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Januari 13,2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, ukaguzi huo ulilenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi kwa kuthibitisha kuwa magari yote yanayotumika kuwabeba yako katika uimara na umadhubuti wa mifumo muhimu ikiwemo usukani, tairi, bodi, injini, breki, mikanda ya usalama pamoja na viti.

Kamanda Maigwa amesema katika ukaguzi huo, jumla ya magari 201 ya shule yalikaguliwa kati ya hayo 180 yalibainika kuwa katika hali nzuri ya kuendelea kutoa huduma, huku 21 yakionekana kuwa na ubovu mbalimbali na hivyo kuzuiwa kufanya kazi.

“Wamiliki na madereva wa magari hayo mabovu wameelekezwa kuyafanyia matengenezo na kuyarejesha tena kwa ajili ya ukaguzi wa pili (re-inspection) kabla ya kuruhusiwa kuendelea kutoa huduma”amesema Kamanda Maigwa.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo limeendelea na ukaguzi wa vyombo vya moto kwa kutumia mfumo wa MIMIS (Motor Vehicle Inspection Management Information System), pamoja na utoaji wa stika za usalama barabarani kwa njia ya kielektroniki.

Amesema ukaguzi huo unahusisha magari binafsi, ya biashara, pamoja na pikipiki za magurudumu mawili na matatu.

“Katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba 13, 2025 hadi Januari 13, 2026, jumla ya magari 17,241 yamekaguliwa mkoani hapa. Kati ya hayo  binafsi ni 9,266, ya biashara 7,619, na pikipiki za magurudumu mawili na matatu ni 2,000”.

Jeshi la Polisi limewataka wamiliki wa vyombo vya moto kuzingatia matakwa ya kisheria na kuhakikisha magari yao yanakuwa salama wakati wote, ili kuendelea kulinda maisha ya watumiaji wa barabara, hususan watoto wanaotegemea usafiri wa shule.

Wakizungumza baadhi ya wananchi mjini Moshi, wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kufanya ukaguzi wa magari ikiwemo ya shule, wakieleza kuwa hatua hiyo itawezesha wanafunzi kusafiri katika hali salama.

“Ukaguzi wa magari ni jambo la msingi sana niombe polisi ukaguzi huo ufanyike mara kwa mara ili kudhibiti magari mabovu ambayo yamekuwa yakibeba wanafunzi. Lakini pia ukaguzi huo ufanyike hata barabarani asubuhi kuangalia idadi ya wanafunzi kwenye hayo magari, kwani mengine hubeba wanafunzi wengi kupita uwezo wa magari” amesema Rose John.

Naye Enos Manja amesema ukaguzi wa magari ya shule ni muafaka wa kulinda usalama wa watoto na kuomba ufanyike mara kwa mara.

“Hatua hii ni muafaka kwa sababu inalinda usalama wa watoto, ukaguzi huu uwe unafanyika mara kwa mara na si kusubiri kipindi cha kufungua shule, ili kuhakikisha magari yote yanayobeba wanafunzi yanakuwa na usalama katika mifumo yake yote kwa kipindi chote, “amesema Masanja.