Rais Samia aitwisha mzigo Mahakama Dira ya Taifa 2050

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wakati Taifa likielekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050, mhimili wa Mahakama una nafasi muhimu wa kujenga Taifa lenye haki, amani, usalama na utulivu.

Rais Samia ameeleza hayo leo Jumanne Januari 13, 2026 wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), uliofanyika viwanja vya makao makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Amefafanua Dira ya Taifa ya 2050, imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, amani, usalama na utulivu na imefafanua kuwa utawala bora na utawala wa sheria ni msingi wa maendeleo endelevu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Matukio tofauti ya picha aliposhiriki ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama Cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika Makao Makuu ya Mahakama Mkoani Dodoma leo January 13,2026.

“Jambo hili haliwezekani pasipo kuwepo na Mahakama imara na iliyoaminika na wananchi wake, na Serikali tunaelekea kujenga mahakama hiyo,” amesema.

Amesema ili kufikia azma hiyo, Serikali imeshachukua hatua kadhaa na itaendelea kuchukua ili kuijenga Mahakama imara inayotoa haki kwa wananchi wake.

Amesema hivi karibuni Serikali ilipitisha mpango wa muda mrefu wa utekelezaji wa dira hiyo, akisema ndani yake asilimia 22 ya mambo yafanywa na Serikali huku asilimia 70 yatafanywa na sekta binafsi kwa ushirikiano na Serikali na asilimia nane yatafanywa na mashirika ya umma.

Rais Samia ameeleza katika hali kama hiyo, Mahakama ina kazi kubwa ya kufanya ikiwemo kusimama imara katika mchakato wa haki.

“Tunaposema asilimia 70 tutashirikiana baina ya Serikali na sekta binafsi, tunatarajia kuialika sekta binafsi ya dunia yote kuja Tanzania. Katika hili tunapoendelea mbele tutapata migogoro mingi ya mikataba ya kazi, ya kodi na ya utekelezaji wa mikataba yenyewe.”

“Sasa haya yote tutategemea Mahakama yetu ya Tanzania isimame katika matawi yake, lakini isimame katika kutetea haki ya Watanzania na Taifa. Hivyo Mahakama tunawategemea nanyi ni mhimili muhimu sana katika utekelezaji wa Dira ya Taifa,” ameeleza.