Serikali ya Gambia kuwalipa fidia walionyanyaswa na ‘Rais dikteta’

Gambia. Tume ya Fidia ya Gambia imeanza kuwalipa fidia kwa waathiriwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu uliotekelezwa chini ya utawala wa aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo na Rais wa mpito kuanzia 1994 hadi 2017, Yahya Jammeh.

Tume hiyo imetoa taarifa yake Jumatatu Januari 12, 2026, ikielezea kuwa hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa jukumu lake la kuhakikisha haki na heshima kwa waathiriwa.

Tume hiyo  imesema malipo ya fidia yanatolewa kwa awamu, yakianza na waathiriwa waliopitia ukiukwaji wa haki katika hatua za awali za utawala wa Jammeh.

“Tume inathibitisha dhamira yake ya kutoa fidia kwa uwazi na kwa kuzingatia mahitaji ya waathiriwa, kulingana na mamlaka yake,” imesema taarifa hiyo.

Jammeh, ambaye alikuwa ofisa wa kijeshi, alichukua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1994 na aliendelea kuwa rais hadi mwaka 2017.

Aliingia uhamishoni baada ya kushindwa katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 dhidi ya Adama Barrow.

Utawala wa kiimla wa Jammeh ulikumbwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo mauaji ya kiholela na kukamatwa bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Tume ya Fidia ya Gambia iliundwa mwaka 2017 kwa lengo la kuchunguza ukiukwaji huo, kukusanya ushahidi kutoka kwa waathiriwa na mashahidi na kufanya kazi ya kuleta haki ya mpito na maridhiano ya kitaifa.